NA MWAJUMA JUMA

TIMU za mpira wa Kikapu za  Polisi kwa wanaume na JKU wanawake zimefanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi Kuu ya Zanzibar iliyomalizika juzi.

Polisi imetwaa ubingwa huo mara ya pili mfululizo baada ya hapo juzi kushinda katika mchezo wake wa fainali dhidi ya timu ya Stone Town ambayo aliifunga kwa pointi 58-54.

Katika mchezo huo ambao ulivuta hisia za watazamaji waliokuwepo hapo Polisi licha ya kutwaa ubingwa huo lakini haikuwa kazi ya rahisi kutokana na upinzani walioupata.

 Upinzani wa timu hizo ulianza kuonesha tokea robo ya kwanza ambapo Polisi aliongoza kwa pointi 10-7, wakati robo ya pili ambayo ni ya mapumziko waliongoza kwa kupata pointi 27-23.

 Katika robo ya tatu ya mchezo huo upinzani uliongezeka zaidi na Polisi ambao walikuwa hoi, walicheza kufa na kupona ili kuhakikisha wanashinda kutetea ubingwa wao ambapo robo hiyo ya waliimaliza kwa kuvuna point 44 na wapinzani wao 43.

Hadi filimbi ya kuashiria kumalizia robo ya nne miamba hiyo ilirudi uwanjani kuendelea na mchezo wao, ambao ulimalizika kwa Polisi kuondoka na ubingwa na kwenda kusherehekea  katika kambi yao iliyopo Ziwani.