MAREKANI imempa jukumu kubwa waziri wake wa mambo ya nje, Mike Pompeo ya kuibadilisha taswira ya nchi ya Israel kwa mataifa ya kiarabu ambayo yanaichukulia nchi hiyo adui wao mkubwa.
Kazi hiyo aliyopewa Pompeo ilionekana kama misheni isiyowezekana kwa yashinikiza mataifa ya kiarabu kurejesha mahusiano na Israel, hata hivyo mafanikio yamekuwa machache sana.
Pompeo alifanya ziara tofauti kabisa na nyingine ili kuhakikisha misheni ya kurejeshwa kwa mahusiano kati ya mataifa ya kiarabu na Israel yanafanikiwa, jambo ambalo kwa muda mrefu lilichukuwa kama lisilowezekana kutokana na mkwamo wa kisiasa wa mgogo wa Israel na Palestina.
Hata hivyo, hivi karibuni kabla, kile ambacho kilionekana kutowezekana kikafanikishwa na kuanza kufanya kazi baada ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kukubali kurejesha mahusiano na Israel chini ya muafaka uliosimamiwa na Marekani.
Mpango huo ulisitisha unyakuzi wa ardhi ya Wapalestina inayokaliwa na Israel katika ukingo wa magharibi na kufungua mlango wa mahusiano mapana kati ya nchi hizo mvili, ikiwemo mahusiano kamili ya kidiplomasia.
Kwenye orodha ya nchi alizotembelea Pompeo, hakuna iliyokuwa muhimu zaidi kuliko Bahrain, taifa hilo la kisiwa kwa muda mrefu lilishirikiana na Israel katika maeneo mengi ya manufaa kwa pande zote mbili.
Bahrain ilikuwa moja ya nchi za kwanza katika ukanda wa mashariki ya kati kuukaribisha mpango huo, ambapo wataalamu wengi wanakubaliana kuwa ilikuwa ya pili kwenye orodha ya nchi zinazorejesha mahusiano na Israel.
Hata hivyo, matumaini hayo yalififia wakati Mfalme Hamas bin Isa al-Khalifa wa Bahrain kumueleza Pompeo kwamba nchi yake haitasonga mbele na pendekezo hilo la Marekani.
Badala yake, mfalme huyo alisema Bahrain inaendelea kuunga mkono mpango wa amani ya uarabuni unaoongozwa na Saudi Arabia, ambao unatoa wito wa kuungwa kwa taifa huru la Palestina ndani ya mipaka yake ya kihistoria kwa kubadilishana na kurejesha mahusiano na mataifa ya kiarabu.
Kwa Bahrain, yapo mengi sana ya kupoteza kama itarejesha mahusiano na Israel bila makubaliano mapana ya kikanda na hasa kutoka kwa mshirika wake wa karibu Saudia.
Mtafiti wa masuala ya ghuba katika ofisi ya mambo ya kigeni ya Baraza la Ulaya (ECFR) Cinzia Bianco alisema kusitasita huenda kukachangiwa na sababu kadhaa, ikiwemo wasiwasi wa Saudia kuwa wataonekana kuwa na makosa kama Bahrain itarejesha mahusiano na Israel.
Alisema kama dola kubwa la kikanda na kiongozi wa kidini, Saudia haina uwazi wa kubadilika ambao nchi nyingine ndogo zinao. Kwa hiyo hata kujihusisha kwa karibu na Bahrain kutazusha ukosoaji mkubwa kutoka kwa baadhi ya makundi ya kisunni yenye mafungamano na makundi ya itikadi kali, kisiasa wakiongozwa na Uturuki na Qatar, ambao ni mahasimu wa kikanda wa Saudia.
Wakati harakati za Wapalestina zikiendelea kutengeneza sehemu muhumu katika vuguvugu la umoja wa Kiarabu, watalaamu wanaamini kuwa wengine wachache wanapanga kuufuata mkondo wa UAE.
Bianco wa ECFR, alisema haamini kama muafaka wa UAE na Israel unapisha njia ya kuundwa mahusiano rasmi kati ya Israel na Saudi Arabia, Oman, Qatar au Kuwait.
Alisema katika mataifa hayo, licha ya kuwepo kwa uungwaji fulani mkono kwa suala la Palestina kutoka ndani ya vijana wa Kiarabu, hasa Saudi Arabia, upinzani kuelekea kurejeshwa mahusiano bado upo juu. Kutokana na hilo, mafanikio ya ujumbe wa Pompeo bado hayapatikani, angalau kwa sasa.
Sudan yasema serikali ya mpito haina mamlaka ya kurejesha mahusiano na Israel
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo yuko nchini Sudan,akitokea nchini Israel,kwa ziara ya kwanza ya kiongozi wa juu wa Marekani nchini humo.
Ziara za Pompeo za kuyaomba mataifa ya kiarabu kuanzisha uhusiano na Israel zikamfikisha nchini Sudan, ambapo ilikuwa ziara ya kwanza ya kiongozi wa juu wa Marekani nchini humo tangu kupinduliwa Omar al-Bashir mwaka jana.
Lengo kuu la ziara hiyo ya Mike Pompeo ni kujadili kurejeshwa kwa mahusiano kati ya Sudan na Israel, kufuatia makubaliano kama hayo na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Ndege aliyopanda Pompeo kutoka Tel Aviv hadi Khartoum ilikuwa ya safari ya kwanza ya moja kwa moja baina ya mataifa hayo. Sudan na Israel hazijawahi kuwa na uhusiano wa kidiplomasia.
Pompeo alikutana mjini Khartoum na waziri mkuu Abdalla Hamdok, ambapo Hamdok alisema kwamba walikuwa na mazungumzo ya moja kwa moja na ya wazi pamoja na Pompeo.
Hamdok alisema kwamba wamejadili kuondolewa Sudan kwenye orodha ya nchi zinazofadhili ugaidi, uhusiano baina ya Sudan na Marekani na uungwaji mkono wa Marekani kwa serikali ya mpito ya kiraia.
Sudan inatarajia kuondolewa kwenye orodha ya nchi iliyowekewa vikwazo na Marekani, nchi hiyo inayotegemea usafirishaji wa mafuta, iliwekewa vikwazo vya kiuchumi tangu miaka ya tisini.
Faisal Saleh, msemaji wa serikali ya Sudan alisema kwamba kwenye mazungumzo yao waziri mkuu wa Sudan alimuambia Pompeo kwamba serikali ya mpito haina mamlaka ya kuanzisha uhusiano rasmi na Israel.
Mnamo mwezi Februari, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu alikutana na Jenerali Burhan kwa siri nchini Uganda, ambapo baadaye wawili hao walitangaza kuanza hatua za kurejesha mahusiano kati ya nchi zao.
Chini ya utawala Omar El Bashir, aliyepinduliwa baada ya kuiongoza Sudan kwa miongo mitatu, nchi hiyo ilikuwa na uhusiano wa miaka mingi na kundi la ugaidi la Al-Qaida, lililokuwa likiongozwa na Osama Bin Laden.
Utawala wa Trump unayachukulia makubaliano kati ya Umoja wa Falme za Kiarabu na Israel kuwa ni alama kubwa ya kihistoria kwenye siasa zake za nje, katika wakati huu Trump akiwania kuchaguliwa tena katika uchaguzi wa Novemba mwaka huu.