PARIS, Ufara
MABINGWA wa soka wa Ufaransa, Paris Saint Germain, wametajwa kuwa mbioni kumsajili kiungo wa Arsenal, Matteo Guendouzi.

Arsenal imemuweka sokoni kiungo huyo mwenye umri wa miaka 21, kwa gharama ya pauni milioni 30, na meneja Mikael Arteta amedhamiria kumuuza katika kipindi hiki cha usajili wa majira ya kiangazi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa kwenye gazeti la Football London, PSG wamedhamiria kumsajili kiungo huyo, na wakati wowote watakwenda London kuanza mazungumzo ya kumrejesha nyumbani.
Guendouzi alikuzwa kisoka kwenye kituo cha vijana cha PSG kuanzia mwaka 2005 hadi 2014, na baada ya hapo alijiunga na Lorient.

Miamba hiyo ya ‘Ligue 1’, imekua ikimfuatilia kwa karibu Guendouzi na imeonyesha kuridhishwa na kiwango chake, japo kwa upande wa meneja wa Arsenal, Arteta ameonekana kuwa mchezaji mwenye nidhamu mbovu uwanjani.

Guendouzi aliingia kwenye matatizo na Arteta Juni 20, baada ya kuonyesha utovu wa nidhamu wakati wa mchezo dhidi ya Brighton & Hove Albion, kwa kumkunja mchezaji wa klabu hiyo Neal Maupay, na kisha kumtolea maneno machafu.

Katika mchezo huo, Arsenal walipoteza kwa kufungwa mabao 2-1.
Mbali na tukio hilo, Guendouz alionyesha utovu wa nidhamu mwengine kwa kuandika kwenye ukurasa wake wa Twiter: “Michezo miwili, pointi 6! Najivunia timu yangu.. Turudi kazini @Arsenal.”