PARIS, Ufaransa

MABOSI wa Paris Saint-Germain inayoshiriki Ligue 1 ya nchini Ufaransa wakiwa ni mabingwa kwa msimu uliopita, wamesema wanaamini kuwa wana uwezo wa kuipata saini ya nyota wa Barcelona, Lionel Messi kwa kuwa ameonyesha nia ya kutaka kuondoka.

Licha ya Messi kusema ameghairi maamuzi yake ya kuondoka kutokana na ada ya kuhama ndani ya La Liga kuwa kubwa, bado wana imani ya kuipata saini ya nyota huyo kwa ajili ya msimu ujao.

Messi amesema kuwa kwa sasa hawezi kuondoka ndani ya Nou Camp kwa kuwa ada ya pauni milioni 630 inayotakiwa ili aondoke ndani ya La Liga ni kubwa, na hawezi kuburuzana na mabosi wake mahakamani kwa kuwa anaipenda timu hiyo.

Kwa sasa Messi atabaki kuwa chini ya kocha mkuu, Ronald Koeman kwa ajili ya kuendelea na maisha kwa msimu ujao.

Lakini  PSG imesema kuwa ina uwezo wa kupata saini ya nyota huyo kwa ajili ya msimu ujao kupitia kwa kiongozi wao Leonardo, akifananisha kampeni hizo na kuipata saini ya nyota wa zamani wa Manchester United, David Becham msimu wa 2013.