PARIS, Ufaransa
MABINGWA wa Ufaransa, Paris Saint-Germain imetoa tamko la kumuunga mkono mshambuliaji, Neymar da Silva ‘Junior’, kufuatia tukio la kibaguzi analodaiwa kufanyiwa wakati wa mchezo wa ligi mwishoni mwa wiki iliyopita.

Mchezo huo dhidi ya Olympic Marseille, uligubikwa na vurugu dakika mbili kabla ya kipenga cha mwisho kupulizwa na mwamuzi, huku chanzo kikitajwa ni rafu aliyochezewa mchezaji wa Marseille, iliyochagizwa na maneno ya kibaguzi kwa wachezaji wa timu pinzani.

Tukio hilo lilizua ‘songombingo’ kubwa na kupelekea mwamuzi kutumia usaidizi wa VAR, na baadae kutoa adhabu ya kadi tano nyekundu.

Taarifa iliyotolewa na PSG kupitia kurasa za mitandao ya kijamii ilieleza: “Hakuna nafasi ya ubaguzi kwenye jamii, soka au maisha yetu.

“Tunategemea kamati ya maadili kupitia LFP itafanya uchunguzi wa kina na kutoa majibu sahihi. Klabu ipo tayari kushirikiana na LFP kama itahitajika”.

Neymar amesisitiza amekuwa muhanga wa ubaguzi wakati akiwa mmoja kati ya wachezaji watano walipotolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kutokea masumbwi kwenye pambano hilo.

Nyota huyo raia wa Brazil alionekana akimshutumu Alvaro Gonzalez kwa kumuita kima, katika wimbi la maandishi katika ukurasa wa twitter baada ya kutolewa nje katika dakika za nyongeza kwa kumpiga kibao mlinzi wa Marseille kisogoni.
“Angalieni kuhusu ubaguzi. Ndio sababu nilimpiga,” Neymar, ambaye alikuwa anarejea uwanjani kutoka katika karantini ya virusi vya corona, alisema, wakati akitoka uwanjani.