Barcelona, Hispania

RAIS wa Ligi Kuu ya Hispania, La Liga, Javier Tebas, amesema kuwa kwao ilikuwa ni ngumu kumuachia mchezaji Lionel Messi aondoke.

Messi alitangaza kuondoka kwenye ligi hiyo na kwenda Manchester City, lakini ghafla alibadilisha mawazo na kuamua kubaki kwenye timu hiyo baada ya majadiliano marefu na klabu yake.

 Messi aligoma kufanya mazoezi kwa wiki nzima na Barcelona na kwa sasa baada ya kusitisha mpango wake wa kutaka kuondoka  ameanza mazoezi na wachezaji wenzake.

Rais huyo amesema alipambana mwenyewe kuhakikisha kuwa mshambuliaji huyo bora duniani anabaki kwenye ligi hiyo.

Wakati Messi akisema kuwa anaondoka bure, La Liga walitoa taarifa iliyokuwa ikionyesha kuwa ili kumpata mchezaji huyo unatakiwa kutoa kitita cha pauni milioni 630, sawa na shilingi trilioni 2.

“Kama ligi lazima tulinde sheria na kufuata haki, kila mchezaji lazima aheshimu mkataba wake.

“Ukweli mimi sikuona mpambano kati ya Messi na klabu yake, kwanza natakiwa kumheshimu sana kwenye hilo na jinsi alivyokaa kwenye ligi hii kwa muda mrefu.

 “Namheshimu sana Messi, nampenda sana na historia aliyotengeneza hapa kwa miaka 20 inajionyesha.Nafikiri suala langu lilikuwa kuwa mkataba unaoheshimiwa, lakini vizuri pia ni kwamba walikaa wenyewe na kukubaliana na yote yakaisha, lakini kwangu ilikuwa mgumu kumuona anaondoka kwenye La Liga,” amesema rais huyo.