PARIS, Ufaransa
MWENYEKITI wa Kampuni ya beIN, na ais wa mabingwa wa Ufaransa, PSG, Nasser Al-Khelaifi, anashtakiwa kwa kosa la kumshawishi Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Jerome Valcke, kutenda kosa la jinai na kupokea rushwa.

Mwenyekiti huyo wa Shirika la Habari la BeIN lililoko huko Qatar, ambaye pia ni Ofisa Mwandamizi wa FIFA amekwenda kwenye kesi nchini Uswisi akituhumiwa juu ya kupokea rushwa katika utoaji wa haki za matangazo ya televisheni kwa ajili ya fainali zijazo za Kombe la Dunia (2022).

Nasser Al-Khelaifi,

Al Khelaifi, ambaye yupo pia kwenye kamati kuu ya bodi ya soka ya Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA), ameshtakiwa kwa kumshawishi Valcke kupokea kiasi cha zaidi ya dola za Marekani 1,000,000.

Valcke mwenye umri wa miaka 59, ambaye tayari amefungiwa na kamati ya maadili ya FIFA kwa miaka 10, kwa ukiukaji wa maadili alifika mahakamani juzi akituhumiwa kupokea rushwa, kufanya usimamizi mbaya na kughushi nyaraka.

Wawili hao wanakabiliwa na mashtaka ya jinai juu ya madai kwamba Valcke alitumia nafasi yake kushawishi utoaji wa haki za matangazo ya TV kwa Italia na Ugiriki kwenye fainali kadhaa za Kombe la Dunia na Kombe la Mabara tangu mwaka 2018 hadi 2030.

Waendesha mashtaka wa Uswisi wamekuwa wakichunguza ufisadi unaozunguka FIFA tangu 2015, kipindi ambacho chombo hicho cha kimataifa kilipokuwa kikiingia katika kashfa mbaya zaidi ya ufisadi katika historia yake.

Kashfa hiyo ilisababisha rais wake, Sepp Blatter na Rais wa UEFA, Michel Platini kufungiwa maisha kwenye mchezo huo, wakati maofisa kadhaa walishtakiwa nchini Marekani kwa tuhuma zinazohusiana na ufisadi.(Goal).