NIAMEY, GAMBIA

RAIS wa Gambia Adama Barrow siku ya Alhamis alitoa wito kwa jamii ya kimataifa kusaidia nchi zinazoendelea ambazo uchumi wake umedorora kutokana na COVID-19.

Akiongea kwenye mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa njia ya video, rais Barrow amesema nchi zinazoendelea kama Gambia, zitaendelea kuhitaji uokozi kutoka Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa ili kunusurika na kushuka kwa uchumi.

Alibainisha kuwa uchumi wa Gambia umeshuka kwa asilimia 2, na unaendelea kuporomoka wakati sekta ya utalii, ambayo ni mwajiri mkubwa na inayoingiza fedha nyingi za kigeni, inateketea, huku idadi ya watu wasio na ajira ikiongezeka kwa kasi.

Hivyo alisema kutokana na nchi ndogo na zinazoendelea kusumbuka kusimamia mizigo yao ya madeni huku zikijitahidi kukuza uchumi, ameutaka Umoja wa Afrika upunguze madeni au kuyafuta kabisa, kuongeza upatikanaji wa fedha za kimataifa, kupunguza gharama za utumaji pesa katika nchi za nje na kuongeza mshikamano na ushirikiano duniani.