BAMAKO, MALI

RAIS wa mpito wa Mali na makamu wa rais wameapishwa jana, zaidi ya mwezi mmoja baada ya mapinduzi yaliyofanywa na wanajeshi katika taifa hilo la Afrika magharibi.

Sherehe hiyo ya kuapishwa katika mji mkuu Bamako, ilifanyika wakati Mali inaendelea kuwa katika vikwazo vilivyowekwa na mataifa 15 ya Afrika magharibi, ECOWAS, na huku kukiwa na hali ya sintofahamu juu ya maelezo ya kipindi hicho cha mpito.

Waziri wa zamani wa ulinzi na kanali mstaafu Bah N’Daw ndie rais wa mpito wakati kanali Assimi Goita, kiongozi mkuu wa wanajeshi waliochukua madaraka Agosti 18 katika mapinduzi, ni makamu mpya wa rais wa Mali.

Viongozi hao wawili, pamoja na waziri mkuu ambaye atateuliwa katika siku zijazo, wataongoza serikali ya mpito hadi uchaguzi miezi 18 ijayo.

Rais wa zamani wa Nigeria Goodluck Jonthan amehudhuria sherere hizo kama mwakilishi wa ECOWAS, ambayo imekuwa ikishinikiza kurejeshwa haraka kwa utawala wa kiraia.