NA MWANAJUMA MMANGA
MKUU wa Wilaya ya Kaskazini ‘B’ Rajab Ali Rajab, ameifunga skuli ya maandalizi ”Amish marafiki Kiwengwa” kwa muda wa wiki moja, ili kulitafutia ufumbuzi tatizo la mgogoro ulipo kati ya walimu pamoja na uongozi wa skuli hiyo.
Alisema ameamua kuifunga skuli hiyo kwa muda baada ya kubaini kuwepo kwa matatizo ikiwemo utaratibu wa uajiri wa walimu, ambao wameajiriwa bila ya kufunga mikataba ya kazi, pamoja na kushindwa kufuata taratibu za uanzishwaji wa skuli za maandalizi zilizowekwa na Wizara ya Elimu.
Aliyasema hayo wakati akizungumza na walimu wa skuli hiyo waliofika huko ofisini kwake huko Mahonda kwa ajili ya kupeleka malalamiko yao.
Alisema serikali haikatazi jamii kuanzisha skuli, hivyo ni vyema kwa wanaoanzisha kuzingatia taratibu zilizowekwa na Wizara husika, ili kuepusha migogoro, kwani endapo sheria na taratibu zitazingatiwa zitasaidia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi bila ya usumbufu wowote.
Alisema kwa mujibu wa sheria za Wizara ya Elimu ni jukumu la kila skuli kuanzisha kamati ili iweze kushirikiana na uongozi wa pindi yanapotokea matatizo kama hayo.