LISBON, Ureno
NYOTA wa Ureno, Cristiano Ronaldo, amelilinganisha soka katika viwanja vitupu visivyokuwa na mashabiki kama kwenda kwenye sarakasi bila na kuwa na vazi rasmi la kuchekesha.

Mshambuliaji huyo alifunga goli lake la 100 na 101 kwa nchi yake katika ushindi wa magoli 2-0 dhidi ya Sweden juzi katika ligi ya soka ya mataifa.

“Ni kama kwenda kwenye sarakasi bila mchekeshaji aliyevalia vazi la kuchekesha, kwenda kwenye bustani bila ya maua”, alisema, Ronaldo na kuongeza,
“Hatupendi kama wachezaji, lakini, tayari nimezoea. Ninatafakari kabla ya mechi tayari nikijua kuwa uwanja utakuwa mtupu”.

Ronaldo alisema amekosa hata mashabiki wapinzani. “Inasikitisha”, alisema, mshambuliaji huyo wa Juventus ya Italia.

“Ninapenda wakati ninapodhihakiwa katika mechi za ugenini, inanipa motisha. Lakini suala la afya linatakiwa kupewa kipaumbele na tunahitaji kuheshimu hilo. Lakini inasikitisha.”

Aidha, Ronaldo, alisema, ana matumaini kuwa ndani ya miezi michache mashabiki wanaweza kurudi viwanjani kwa sababu wao ndio furaha ya mchezo wa soka.Kwa magoli yake dhidi ya Sweden, Ronaldo amekuwa mchezaji wa pili tu wa kiume kufikia magoli 100 katika mpira wa miguu wa kimataifa. Anamfuatia tu mshambuliaji wa zamani wa Iran, Ali Daei, ambaye aliifungia timu yake ya taifa mabao 109.(Goal).