NAIROBI,KENYA
NAIBU wa Rais William Ruto amekashifu mienendo ya baadhi ya watumishi wa umma kutumia nafasi zao za uongozi kujibizana vikali badala ya kuwatumikia wananchi.
Akizungumza katika eneo la Athi River wakati wa ibada ya Kanisa la Kianglikana, Ruto alisema viongozi waliochaguliwa katika chama tawala cha Jubilee wanafaa kuhakikisha wanatekeleza ahadi walizotoa kwa wananchi wakati wa kampeni.
Katika kauli inayofikirika kumjibu Waziri wa Mazingira Keriako Tobiko ambaye alimlaumu Ruto kwa madai ya kuhujumu mipango ya Rais Uhuru Kenyatta, Naibu wa Rais alisema sasa si wakati kuoneshana ubabe ilhali wananchi bado wana mahitaji mengi ya kushughulikiwa.
Wakati huo huo, Ruto aliwashauri wanasiasa wa vyama mbalimbali kujiepusha na siasa za uchochezi ili kuwaunganisha wananchi.
Kauli ya Ruto inajiri siku mbili tu baada ya Waziri Tobiko kujibizana vikali na Aliyekuwa Kiongozi wa Wengi katika Seneti Murkomen, kuhusu ufanyaji kazi wa Serikali na misukosuko inayoshuhudiwa ndani ya Jubilee kuelelekea uchaguzi mkuu ujao.
Ruto aliandamana na wandani wake wa eneo la Ukambani ambao walikuwa wakimpigia debe kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.