KIGALI,RWANDA

MTU ambaye mchango wake katika kuwaokoa watu wakati wa mauaji ya halaiki nchni Rwanda ulienziwa katika filamu ya Hotel Rwanda, yuko korokoroni nchini Rwanda, kwa tuhuma za ugaidi.

Kitengo cha kuendesha mashitaka nchini humo kilisema mtu huyo, Paul Rusesabagina alikamatwa nje ya nchi kwa ushirikiano wa kimataifa.

Kitengo hicho, RIB kimemuonyesha Rusesabagina mbele ya waandishi wa habari,kimesema anashukiwa kuanzisha na kufadhili kundi lenye silaha, linaloendesha shughuli yake katika ukanda wa maziwa makuu.

Rusesabagina ambaye alituzwa tuzo nyingi za Haki za Binadamu, ikiwemo Tuzo ya Rais wa Marekani ya uhuru mwaka 2005, amekuwa akiikosoa vikali Serikali ya Rais Paul Kagame kutokea uhamishoni.

Filamu ya Hotel Rwanda ya mwaka 2004, ilizungumzia mchango wake katika kuwanusuru watu zaidi ya 1200 waliokuwa wakisakwa na wanamgambo wa Interahamwe.