NA KHAMISUU ABDALLAH

DEREVA aliyeshindwa kuifikisha gari yake mwisho wa kituo, Salum Juma Ussi (27) mkaazi wa Bububu wilaya ya Magharibi ‘A’ Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, amefikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.

Mshitakiwa huyo alifikishwa katika mahakama ya mwanzo Mwanakwerekwe mbele ya Hakimu Suleiman Jecha Zidi na kusomewa shitaka la kukatisha ruti ya njia na Mwendesha Mashitaka Koplo wa Polisi Time Said.

Alidaiwa kuwa Juni 30 mwaka huu saa 1:45 asubuhi huko Mwanakwerekwe akiwa dereva wa gari yenye namba za usajili Z 187 KH inayoenda njia 538 akitokea Amani kuelekea Fuoni alipofika Mwanakwerekwe sokoni aligeuza gari yake na alitakiwa kufika fuoni kama ruti yake ya njia inavyoelekeza kitendo ambacho ni kosa kisheria.

Kosa la kukatisha ruti ya njia ni kinyume na kifungu cha 205 (2) (a) na kifungu cha 201 (1) cha sheria namba 7 ya mwaka 2003 sheria za Zanzibar.

Mshitakiwa huyo aliposomewa shitaka hilo alilikubali na kuiomba mahakama imsamehe kwa madai kuwa ndio kosa lake la mwanzo huku upande wa mashitaka ukidai kuwa hauna kumbukumbu ya makosa ya zamani kwa mshitakiwa huyo mahakamani hapo hivyo adhabu itolewe kwa mujibu wa shitaka alilopatikana nalo.

Hakimu Suleiman alimtia hatiani mshitakiwa huyo na kumuona ni mkosa kisheria na kumpa adhabu ya kulipa faini ya shilingi 30,000 na akishindwa atatumikia Chuo cha Mafunzo kwa muda wa mwezi mmoja.

Mshitakiwa huyo alilipa faini hiyo ili kujinusuru kwenda Chuo cha Mafunzo kwa muda huo.