NA MWANDISHI WETU MOROGORO

MGOMBEA Mweza wa Chama cha Mapinduzi, Samia Suluhu Hassan, amewataka wananchi wa Morogoro kujiandaa kupokea mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo katika serikali ijayo.

Hayo aliyasema wakati akiwahutubia wananchi, katika kampeni za Chama cha Mapinduzi, zilizofanyika Mvumero Mkoani Morogoro.

Samia alisema endapo wananchi wa Mkoa huo watakichagua Chama cha Mapinduzi, katika uchaguzi ujao serikali imejipanga kuona inakuza sekta ya kilimo kwa kufanya mageuzi makubwa kwa kuimarisha uzalishaji wa mazao mbali mbali.

Alisema Morogoro imekuwa ikijizolea sifa ya kuzalisha sukari katika kiwanda chake cha Mtibwa, na serikali itahakikisha inaweka mazingira bora kwa wawekezaji, ili Tanzania iwe na tija inayotakikana katika uzalishaji wa chakula cha ndani na biashara.

Alisema katika utekelezaji wa ilani iliyopita katika Mkoa huo serikali iliweza kufanya Ukarabati wa jumla ya skimu 17 ambazo zimekamilika na ukarabati unaendelea kwa skimu tano za umwagiliaji.

 Akizitaja skimu hizo alisema ni Mbogo na Kigugu (Mvomero), Msolwa Ujamaa na Njage (Kilombero) na Mvumi (Kilosa) ambao unaendelea ikiwa ni pamoja na ukarabati wa miundombinu ya barabara (feeder roads).

Kutokana na hali hiyo, Samia alisema wananchi wa Mkoa huo watarajie makubwa yanakuja katika kuibadili sekta ya kilimo, huku serikali ikiingia madakani itaimarisha huduma za kijamii ikiwemo ya afya.

Alisema serikali inakusudia kuwapatia watanzania wote bima ya afya ikiwa ni hatua itayomsaidia mwananchi kukimbia gharama za matibabu kutokana na hivi sasa kuwa kubwa, jambo ambalo huwafanya kushindwa kumudu gharama zake.

Alisema mpango mpya wa serikali ijayo ni kuona inaongeza ujenzi wa vituo vya afya, ili viwe vyenye viwango bora pamoja na kujenga hospitali 98 za Halmashauri.