RIYAD,SAUDIA ARABIA

MATAIFA  29 ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, yamewakosoa watawala wa Saudi Arabia kwa ukiukaji wa haki za binadamu, sambamba na kutaka kuwajibishwa utawala wa Aal-Saud kwa mauaji ya kikatili aliyofanyiwa mwandishi wa habari na mkosoaji mkubwa wa Riyadh, Jamal Khashoggi.

Akisoma taarifa ya pamoja na mataifa 29 mbele ya taasisi hiyo ya juu zaidi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, Balozi wa Denmark, Carsten Staur alisema,kuna haja ya kuwajibishwa watu wote waliohusika na mauaji ya Khashoggi.

Taarifa hiyo ilitolewa siku chache baada ya Mahakama ya Saudi Arabia kuwafutia adhabu ya kifo wahusika wa mauaji hayo ya mwaka 2018 mjini Istanbul nchini Uturuki.

Hata hivyo, watuhumiwa watano wa mauaji hayo walihukumiwa kifungo cha miaka 20 jela, huku wengine watatu wakihukumiwa vifungo vya kati ya miaka saba hadi kumi jela.

Taasisi za UN na mashirika ya kutetea haki za binadamu duniani yalisema hukumu hiyo ni sawa na kuudhihaki mfumo wa sheria.

Mbali na kukosoa mauaji ya kinyama ya Khashoggi, mataifa hayo 29 yalilaani vikali ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaoendelea kushuhudiwa Saudia, katika taarifa yao mbele ya Baraza la Haki za Binadamu la UN.

Taarifa hiyo ilisema wanaendelea kusikitishwa na ripoti kutoka Saudi Arabia za ukandamizaji, watu kupotezwa, raia kufungwa jela kinyume cha sheria huku wafungwa wakinyimwa haki za msingi kama dawa na matibabu, na hata kuzuiwa kuwasiliana na jamaa zao.

Balozi wa Denmark katika Umoja wa Mataifa, Carsten Staur aliongeza kuwa, ingawaje wanakaribisha hatua za mageuzi zilizopigwa hivi karibuni nchini Saudia kama vile kufutwa adhabu ya kifo kwa watoto wadogo, lakini wangali wanatiwa wasiwasi na mwenendo wa kutishiwa maisha, kukamatwa ovyo na kuzuiliwa kinyume cha sheria kwa wanahabari, wakosoaji na wanaharakati nchini humo.