NA KHAMISUU ABDALLAH

WIZARA ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji imetiliana saini makubaliano ya huduma ya mtandao na kampuni ya Zanlink ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa bei nafuu.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mustafa Aboud Jumbe, aliyasema hayo wakati akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika ofisi za wizara hiyo zilizopo Kisauni wilaya ya Magharibi ‘B’ Unguja.

Jumbe alisema mawasiliano ya ‘internet’ ni muhimu kwa wananchi wa Zanzibar hasa kwa wafanyabiashara ambao wanatumia kwa kurahisisha shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Alisema kipindi hiki ambacho baadhi mataifa yanakabiliwa na maradhi ya corona, wafanyabiashara wa Zanzibar wanaagiza biashara kupitia mawasiliano ya mtandao bila ya kusafiri.

“Sekta ya mawasiliano ni muhimu katika kurahisisha mawasiliano na utoaji huduma mbalimbali nchini na kurahisisha maisha ya watu”, alieleza Jumbe.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Miundombinu ya TEHAMA Zanzibar, Mhandisi Shukuru Awadhi Suleiman alisema Zanlink ni wadau wakuu wa miundombinu wa mawasiliano toka serikali ianze biashara ya mkonga wa taifa ambao umeondoa changamoto ya mawasiliano ya internet.

Hivyo, aliitaka kampuni hiyo kuiangalia jamii kwa sababu baadhi ya jamii hawana mawasiliano ya ‘internet’ hivyo kuunga mawasiliano hayo ya mtandao katika vituo vya TEHAMA kwa jamii ili iweze kufaidika.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Zanlink, Sanjay Raja aliipongeza wizara hiyo kwa kuipa fursa kampuni yao kuweza kuutumia mkonga wa taifa ili kuona mawasiliano ya ‘internet’ yanawafikia wananchi.

Alisema kuwa uchumi wa sasa unategemea mtandao wa ‘internet’ hivyo wataitumia fursa hiyo ili kuweza kuwafikia walengwa wengi kuitumia huduma hiyo ili kuweza kukuza uchumi.