NA FATMA AYOUB, MCC
WAZAZI wametakiwa kuacha dhana potofu kuhusu Chanjo za sindano za ‘Tetnas Toxide’ (T T) wanazo pigwa wanafunzi maskulini kwani hazina madhara yoyote.
Kauli hiyo imetolewa na Ofisa kitengo cha kutoa Elimu ya Afya Mwanaisha Abrahmani Mwarabu, alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi huko Ofisini kwake Sogea Mjini Unguja.
Alisema baadhi ya Wazazi wamekuwa na tabia ya kuwakataza watoto wao na kuwa na fikra potofu juu ya suala hilo kwa kudai zinasababisha kutolewa kizazi jambo ambalo sio la kweli.
Aliyasema hayo kufuataia malalamiko ya wazazi kwa kuwakatalia watoto wao kuchomwa sindano hizo kwa kudai zina madhara katika uzazi .
Alifahamisha dhumuni la kuchomwa sindano hizo ni kukinga na maradhi mbali mbali, ikiwemo Pepopunda na kupunguza makali pindi atakapo jichoma mtoto kitu ncha huenda kina ‘tetnasi’.
Nae Kilipo Haji Mjaka kutoka katika kitengo hicho hicho alifahamisha kuwa Sindano hizo pia zinajumuisha na wanazo pigwa wajawazito ambazo ziko tano zinazopigwa kwa wakati tofauti, ili kukinga na matatizo mbali mbali yatakayo jitokeza katika mimba.
Kilipo, alisema pindi Mwanafunzi anapo pigwa sindano hizo anapewa kibali ambacho hata anapofika kupata ujauzito atatatumia kibali hicho, ili kujulikana kama alishawahi kuchomwa.
Aliwataka wazazi kumaliza sindano hizo zote kwa mujibu wa mpangilio wake unavyo sema.