NAIROBI, KENYA

WAKENYA huenda wakakabiliana na hali ngumu baada ya serikali za kaunti kusitisha utoaji wa huduma mikoani kutokana na uhaba wa fedha na wafanyakazi wake kuchukua likizo ya wiki mbili.

Hali hiyo inatokana na kuwepo mzozo wa ugavi wa fedha kwa serikali za kaunti ambao umekosa suluhu baada ya baraza la senate kufanya vikao 10 bila ya kupata utatuzi wa mgogoro huo.

Taarifa kutoka nchini humo zinaeleza kuwa pamoja na maseneta kukutana katika vikao hivyo, wameshindwa kuafikiana kuhusu mfumo wa ugavi wa fedha kwenye kaunti kwa kuzingatia idadi ya wakaazi na ukubwa wa kaunti.

Mwenyekiti wa baraza la magavana, Wycliffe Oparanya, alisema kilichochangia hatua hiyo ni uhaba wa nyenzo na vitendea kazi baada ya maseneta kushindwa kufikia muafaka wa ugavi wa fedha za kaunti.

Gavana Oparanya ameonya kuwa serikali za kaunti zinakabiliana na hali ngumu kutokana na kukosa fedha na wanashindwa kulipa mishahara ya watumishi sambamba na kutoa huduma kwa wananchi.

Naye gavana wa Makueni, Kivutha Kibwana na wa West Pokot John Lonyang’apuo wanamuunga mkono mwenyekiti wa baraza lao kwa kuchukua hatua ya kusitisha huduma za kaunti.

Kwa sasa vituo vya afya vinavyosimamiwa na kaunti havitatoa huduma kwa wagonjwa wa kulazwa na watakaohudumiwa ni wachache wanaohitaji usaidizi.

Kadhalika wafanyakazi wa kaunti wa huduma zisokuwa za msingi wameagizwa kwenda likizo kwa wiki mbili.