MADRID, Hispania
MABINGWA wa Ligi ya Europa, Sevilla CF wamekamilisha dili la kumnyakua beki wa kushoto raia wa Argentina, Marcos Javier Acuna akitokea Sporting CP ya Ureno.

Sevilla inayoshiriki Ligi Kuu ya Hispania ‘La Liga’, imemsajili beki huyo mwenye umri wa miaka 28 ili kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Sergio Reguilon aliyerejea Real Madrid.


Reguilon alijiungana Sevilla kwa mkopo msimu uliyopita na kufanikiwa kutwaa taji la Ligi ya Europa, hali ambayo iliwatamanisha viongozi wa klabu hiyo kutaka kumsajili moja kwa moja, lakini, Real Madrid waligomea dili hilo.

Acuna amejiunga na Sevilla kwa ada ya euro milioni 10 na tayari amekamilisha utaratibu wa kupimwa afya.

Beki huyo alitumia misimu mitatu na miamba ya Ureno, Sporting CP na kucheza mechi 134 katika mshindano yote.

Acuna ambaye aliwahi kuitumikia timu ya taifa ya Argentina katika michezo 27 na kufunga mabao mawili, anakuwa mchezaji wa tano kusajiliwa na Sevilla CF katika kipindi hichi, akitangiliwa na Ivan Rakitic kutoka Barcelona, Oscar Rodriguez wa Real Madrid, Yassine Bounou kutoka Girona na Jesus Fernandez ‘Suso’.

Sevilla ilimaliza katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ‘La Liga’ msimu wa 2019-20 na kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya huku ikitwaa ubingwa wa Ligi ya Europa.
Kwa hatua huyo Sevilla CF itacheza mchezo wa ufunguzi wa msimu mpya wa michuano ya Ulaya (UEFA Super Cup) dhidi ya mabingwa wa soka barani humo, Bayern Munich mnamo Septemba 24.(Goal).