KAMPALA,UGANDA

MEYA wa zamani wa Kampala, Nasser Ntege Sebaggala, maarufu kwa jina la Seya, atazikwa Jumapili wiki ijayo kulingana na wanafamilia wanaosimamia mipango ya mazishi.

Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwao Kisaasi, kitongoji cha Jiji la Kampala,Bwana Muhammed Sebaggala,kaka wa marehemu, alisema waliamua kumzika wiki moja baada ya kufariki kwake, kinyume na utamaduni wa Waislamu kwa sababu watoto wake lazima wawepo kwenye mazishi .

“Ndugu yangu alitaka watoto wake wote wawe kwenye mazishi yake na ndio sababu tumechagua tarehe hii kwa sababu mtoto wake wa mwisho atawasili nchini Jumamosi,” Sebagala alisema.

Seya, alipatwa na mshituko wa moyo katika Hospitali ya Kimataifa ya Kampala Jumamosi asubuhi, kulingana na mdogo wake, Latif Sebaggala, mbunge wa Kawempe North.

Sebaggala alisema ikiwa kuna mabadiliko yoyote ndani ya mpango wa mazishi, kutakuwa na mawasiliano rasmi yatakayotolewa kwa umma kupitia njia tofauti.

“Kifo chake ni pigo kubwa kwa familia na tunataka kumzika kwa heshima, haswa akizingatia kile alichokuwa akitaka kwenye mazishi yake. Ikiwa kuna mabadiliko yoyote katika mipango ya mazishi, tutawajulisha umma kupitia njia za kawaida, ”alisema.