NAIROBI,KENYA

SUALA la sehemu ya mzigo wa msaada wa vifaa vya kukabili Janga la Corona kutoka kwa mfanyabiashara wa Uchina Jack Ma kupotea kabla ya kuwasili nchini Kenya, limeendelea kuibua hisia kinzani wakati wa kikao cha Kamati ya Afya .

Wanachama wa kamati hiyo waliitaka Wizara ya Uchukuzi kufafanua iwapo iliwasiliana na Wakfu wa Jack Ma kuhusu shehena ishirini na moja ya mzigo uliopotea, ili kuwafahamisha Wakenya kufuatia madai ya ufisadi yaliyoibuliwa.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Utawala wa Wizara ya Uchukuzi Chris Obure alisema Serikali ya Kenya haijawasiliana na Jack Maa hadi sasa, hali ambayo imewachochea wanakamati hiyo akiwamo Joshua Kutuny kukashifu utendaji kazi wa Wizara hiyo.

Aidha,Obure alisema suala la kuwasiliana na Jack Maa linaweza kushughulikiwa vyema na Wizara za Afya ikishirikiana na ya Masuala ya Nchi za Kigeni.

Kuhusu swali la mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Afya Sabina Chege iwapo mashirika ya binafsi yalihusishwa wakati wa kusafirisha vifaa hivyo kutoka Uwanja wa Ndege wa Kiamtaifa JKIA, Obure alisema ni mamlaka ya KEMSA pekee iliyohusika katika mchakato huo.

Awali Obure aliiambia kamati hiyo kwamba thamani ya vifaa vilivyopotea haijulikani kwa sasa, na kwamba vilipotea wakati vilipopakiwa kuja Kenya kutoka Addis Ababa nchini Ethiopia, kwenye kituo cha Kudhibiti Maradhi CDC Barani Afrika.

Kwa sasa kamati hiyo inawahoji wakuu wa KEMSA na wasimamizi wa bodi ya mamlaka hiyo ili kueleza zaidi jinsi vifaa vya Msaada wa Jack Ma vilivyosambazwa.