NAIROBI,KENYA

UKAGUZI wa matumizi ya fedha za kukabili janga la corona kwenye Kaunti ya Mombasa unaendelea.

Shughuli hiyo inaendeshwa na Shirika la Kutetea Haki za Kibinadamu la Haki Afrika kwa ushirikiano na mashirika ya Amkeni Wakenya  na  Umoja wa Mataifa la Mipango na Maendeleo UNDP.

Ukaguzi huu unafanywa kwenye miradi yote iliyoanzishwa na Serikali ya Kaunti ya Mombasa katika juhudi za kukabili maambukizi zaidi tangu kisa cha kwanza cha corona mjini Mombasa kilipotangazwa.

Maofisa wa Haki Afrika waliopewa mafunzo ya jinsi ya kuendesha shughuli hiyo wamekuwa wakitembelea maeneo mbalimbali likiwemo eneo la Kivuko cha Likoni Feri ambapo kuna sehemu maalumu ya kupuliza kemikali ya kuua viini kwa abiria kabla ya kusafiri kuelekea ng’ambo ya pili.

Aidha ukaguzi huo unalenga kubaini fedha zilizotumika katika kutengeneza eneo hilo na idadi ya vitanda katika Hospitali ya Coast General na vipumuzi pamoja na  mavazi ya wahudumu wa afya wanaowahudumia wagonjwa wa Covid-19.

Kwa mujibu wa taarifa ya Haki Afrika, maofisa wake watazuru Chuo cha Technical University of Mombasa kukagua sehemu iliyotengwa kuwashughulikia wagonjwa wa Covid-19, vitanda na vifaa vyote vilivyonunuliwa.

Aidha ukaguzi huo utafanyika katika kila Eneo kubaini idadi ya watu walionufaika na misaada mbalimbali kutoka  Serikali ya kaunti wakati huu wa janga la corona kisha kulinganishwa na kiwango cha fedha kilichotumika kufanikisha mpango huo.

Waziri wa Afya wa Kaunti ya Mombasa Hazel Koitaba alisema wameafikiana na mashirika hayo kufanya ukaguzi katika Sekta ya Afya na kisha kutoa ripoti yake. 

Katika kila eneo bunge, maofisa watano watawahojiwa wakaazi mia tatu na hamsini katika kila eneo hilo kuhusu jinsi Serikali ya kaunti hiyo inavyoendelea kukabili janga la corona maoni ambayo vilevile yatajumuishwa kwenye ripoti ya mwisho ambayo itakabidhishwa wadau wanaohusika katika vita dhidi ya corona.

Aidha utalenga kubaini utayari wa kaunti hiyo kukabili maambukizi hasa ikizingatiwa kwamba, hivi karibuni Kaunti ya Mombasa imekuwa ikirikodi idadi ya juu ya watu wanaoambukizwa virusi vya corona.

Hayo yanajiri huku ripoti ya madai ya wizi wa fedha za corona katika Mamlaka ya Kusambaza Dawa KEMSA ikikabidhiwa Mkurugenzi Mkuu wa Mashitaka ya Umma DPP Noordin Hajj, ambayo iwapo itaidhinishwa basi wahusika wote kwenye ripoti hiyo watakamatwa na kufunguliwa mashitaka.