NA LAYLAT KHALFAN

SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC), limewataka waandishi wa habari nchini,kuzifanyia utafiti habari za vyama vya wafanyakazi kabla ya kuzitoa ili kuepusha matatizo yanayojitokeza katika jamii.

Mwenyekiti wa Shirikisho hilo, Ali Mwalimu Rashid, aliyasema hayo wakati akifungua mafunzo kwa waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari, mafunzo ambayo yalifanyika katika ukumbi wa Visitor Inn, Jambiani Mkoa wa Kusini Unguja.

Alisema kuna baadhi ya jamii wanadai kuwa shirikisho la wafanyakazi lipo kwa ajili ya kula pesa zao na hawana kazi yoyote , hivyo ni vyema kuweka usahihi na kufanya utafiti pale wanapotoa habari na kuondoa sumu iliyopo.

Alisema endapo waandishi watafanya utafiti na kufuata maadili ya kazi yao itasaidia jamii kuliamini shirikisho hilo juu ya  kile kinachoripotiwa kwa kua na usahihi katika kuwaelimisha jamii bila ya kuleta sitofahamu.

Aidha, alifahamisha kua, kazi za vyama vya wafanyakazi zipo kila mahali, hivyo aliwashauri waendelee kuibua habari mbalimbali za shirikisho ili kuliletea maendeleo imara siku hadi siku.

Mwalimu alieleza kua, vyombo vya habari vina ushawishi na umuhimu mkubwa wa kufikisha taarifa kwa jamii, hivyo hakuna budi taasisi zote za binafsi na serikali kuviunga mkono ili kufikisha taarifa zinazoaminika  nchini.

Naye Mratibu Miradi wa Shirikisho hilo, Salim Ali Salim, alisema ni vyema kwa vyombo vya habari kushirikiana na vyama vya wafanyakazi ili kujua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi sambamba na kutoa taarifa zilizokua sahihi.

Mapema Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Khamis Mwinyi, alivipongeza vyombo vya habari vya Zanzibar kwa kazi kubwa wanayoifanya wakati wakiwa katika majukumu yao.

Aidha, alisema wakati umefika sasa kwa waandishi wa habari kuendelea na jitihada hizo ili kuimarisha utendaji wa kazi zao katika kuwatetea wafanyakazi na kujua sheria za kazi katika sehemu zao za kazi.

Shirikisho la Vyama vya wafanyakazi Zanzibar (ZATUC), limetoa mafunzo ya siku mbili yenye lengo la kuwaelimisha na kuwajengea uwezo waandishi juu ya taarifa zinazohusu wafanyakazi nchini.