MCHAKATO wa kampeni za kisiasa tunaoendelea nao ni hatua muhimu ya kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 mwaka huu, ambao utahitimika kwa kutupatia Rais mpya wa Jamhuri ya Muungano, Rais mpya wa Zanzibar, wabunge, wawakilishi na madiwani.

Kampeni ni fursa muhimu kwa vyama kukutana na wananchi na wanachama wao kwa kuwatambulisha wagombea wa ngazi mbalimbali sambamba na kueleza yale watakayoyafanya endapo watashinda nafasi wanazoomba.

Kwa upande wa wananchi na wanachama wa vyama vya siasa, hatua ya kushiriki kwenye mikutano ya kampeni ni muhimu zaidi, kwani itawapa fursa ya kuwapima sio kimaneno tu bali kiuwezo viongozi wanaowania nafasi mbalimbali.

Waatalamu wa mambo ya mawasiliano wanatueleza kuwa ili mtu aweze kufanya uamuizi mzuri zaidi, lazima awe na taarifa kamili na za uhakika, kabla ya kufanya uamuzi anaotaka kuuchukua.

Kwa kawaida haitarajiwi mtu asiye na taarifa kamili na za uhakika akafanya uamuzi mzuri na kwamba atarajiwe kwenda kufanya maamuzi yatakayotokana na kufuata mikumbo ya watu na si hasha kuishia kwenye majuto.

Tunachomanisha ni kwamba kabla ya siku ya kupiga kura Oktoba 28 mwaka huu, wananchi wautumie muda huu kushiriki kwenye mikutano ya kampeni kwani itawawezesha kuwa na taariza nzuri na za uhakika.

Tunachosisitiza ni kwamba kama wananchi wana nafasi ni vyema wakashiriki na kufuatilia mikutano ya vyama vyote vya siasa, kwani hiyo itawapa fursa kuweka mizani sawa ya sera na ilani za vyama.

Ni muhimu kwa wanasiasa wakati huu wakiwa wana nadi sera zao majukwaani wakahakikisha kuwa wananchi wa Zanzibar pamoja na yote wanayoyaeleza, kitu cha msingi wanachokitaji kuhakikishiwa kudumu kwa amani yao.

Kwa wananchi wa Zanzibar si muhimu sana kuelezwa kuwa mifereji itatoka maziwa ama asali ama chakula chao cha mchana kitakuwa mana wa-saluwa, kwani itakuwa vigumu kula vyakula hivyo wakati nchi ina machafuko.

Kiukweli amani ikivunjika pengine kutokana na kauli za wanasiasa zinazotoka kwenye viwanja vya kampeni za kisiasa, hakutakuwa na starehe ya kula vyakula hivyo hata kama ni vitamu na tunu kwa wananchi.

Itapendeza sana wakati mifereji ikitoka maziwa na asali pamoja na mambo mengine mazuri watakayoyapata baada ya uchaguzi mambo hayo wakatumia nchi ikiwa na amani. 

Wanasiasa wakumbuke kuwa endapo watakuwa wavivu wa kufikiri kiasi cha kauli zao kuhatarisha amani na kuchochea vurugu kitakacho shuhudiwa ni wimbi la wanawake na watoto kupigania roho zao kwa sababu uzoefu unaonesha kuwa wao ndio waathirika wakubwa wa vurugu na machafuko.

Hatudhani kama kwa wakati huu yupo mwanasiasa hapa Zanzibar anayeweza kutufikisha kwenye hatua hiyo, hata hivyo wanasiasa wanapaswa kuwa makini na kuwajibika kabla ya kuja kutueleza ulimi hauna mfupa.

Aidha tungependa sana kuviomba vyombo vya usalama vikahakikisha vinachukua hatua dhidi ya viashiria vya uvunjifu wa amani, kwani uzoefu unaonesha kuwa baadhi ya gari zinazopakia wananchi wanaokwenda kwenye mikutano ya kisiasa baadhi ya watu wanachukua siala za jadi.

Tutafurahi sana wagombea na vyama vyate wakiwaeleza wananchi kwamba watafanya kampeni za kistaarabu na za kiugwana, bila ya kumtukana mtu, bila ya kushambulia mtu, bila ya kumpaka matope mwengine.

Siasa ni tunda la masimu, lisitugawe, lisitugombanishe, lisitutenganishe. Sisi tunaamini maisha ya amani na utulivu baada ya uchaguzi wa Oktoba 28 yanawezekana.