NA TIMA SALEHE, DAR ES SALAAM

KIKOSI cha Simba kimewasili jana Dar es Salaam kikitokea Mbeya ambapo kilikuwa na mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ihefu FC uliochezwa uwanja wa Sokoine.

Simba imetua  kwenye Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Kambarage Nyererere.Timu hiyo baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 mkoani Mbeya sasa wameanza kuipigia hesabu timu ya Mtibwa Sugar.

Mchezo wao unaofuata dhidi ya Mtibwa Sugar utachezwa Septemba 12 katika uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.

Wataendelea na mazoezi katika uwanja wao wa Simba Mo Arena uliopo Bunju kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo.Kwa upande wa Mtibwa Sugar wao walikutana na  Ruvu Shooting na kuambulia ponti moja baada ya kutoa sare 0-0  kwenye uwanja wa Gairo mkoani Morogoro.

Nao uongozi wa Yanga umewashukuru mashabiki waliojitokeza kwa wingi kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons.Mchezo huo ulichezwa uwanja wa Mkapa na Yanga iligawana pointi mojamoja.

Bao la Tanzania Prisons lilipachikwa kimiani na Lambart Sabiyanka na lile la kusawazishwa kwa Yanga lilipachikwa na Michael Sarpong.

Ofisa Uhamasishaji wa Yanga, Antonio  Nugaz amesema  mashabiki wanahitaji pongezi kwa kujitoa kuiunga mkono  timu yao uwanja wa Mkapa.

“Mashabiki wengi walijitokeza katika hilo tunapenda kuwashuru na kusema asante kwa kujitokeza, ni mwanzo mzuri na imani yetu ni kwamba tutaendelea kujitokeza kwa wingi,” amesema.