NA TIMA SALEHE, DAR ES SALAAM

KLABU ya Simba imetua mkoani Morogoro kujiandaa na mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, dhidi ya Mtibwa Sugar.

Nahodha wa Simba SC, John Bocco,hivi karibuni alizungumza na vyombo vya habari na kusema wanacho kihitaji wao ni pointi tatu katika kila mchezo wao.

Alisema atafurahia kuona malengo yao yanatimia yakufanya vizuri katika kila mchezo na kutetea ubingwa wao.

“Nitafurahi kuona tunafanikiwa kuchukua pointi tatu katika kila mchezo ambao upo mbele yetu yani kama ambavyo tumeanza,”alisema

Wakati huo huo uongozi wa Simba umesema  kwa sasa kikosi kipo tayari kwa ajili ya mechi zote za Ligi Kuu Bara, ikiwa ni pamoja na ile inayosubiriwa kwa hamu na mashabiki dhidi ya Yanga inayotarajiwa kuchezwa Oktoba 18, Uwanja wa Mkapa.

Tayari Simba imemalizana na Ihefu, Septemba 6 kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Sokoine na ilikosa huduma ya wachezaji wake watano ambao walikuwa na sababu mbalimbali.

Gerson Fraga aliyekuwa na matatizo ya kifamilia,Ibrahim Ame aliyekuwa akisumbuliwa na majeraha,Chris Mugalu, Luis Miqussone na Pascal Wawa ambao hawakuwa na mechi ‘fitnesi’.

 Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara alisema wachezaji wote wapo katika hali nzuri na wanaanza maandalizi kwa ajili ya mchezo wao unaofuata dhidi ya Mtibwa Sugar, utakaochezwa Septemba 12, pamoja na mechi nyingine.

“Tunajiandaa vizuri kwa ajili ya mechi zetu zote ikiwa ni pamoja na ile ya wenzentu, sasa taarifa niliyopewa ni kwamba tayari Gerson Fraga yupo Bongo, Ame ambaye alikuwa akisumbuliwa na majeraha naye yupo vizuri’’alisema