NA MWAJUMA JUMA

TIMU za soka za University na Spirit zimefanikiwa kutoka na ushindi katika michezo yao ya ligi daraja la tatu wilaya ya mjini inayoendelea katika hatua ya sita bora.

Ligi hiyo inachezwa katika viwanja vya Mao Zedong kwa nyakati tofauti ambapo University ilicheza na Super Eagle na kuondoka na ushindi wa mabao 2-1, mchezo uliochezwa saa 7:00 mchana Mao Zedong A.

Katika mchezo huo University ambayo ilicheza ikiwa pungufu kufuatia mchezaji wake Hassan Nassir Songoro kutolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu Mohammed Omar katika dakika ya 65, mabao yake yalifungwa na Ali Jecha Ali dakika ya 41 na Abdalla Yussuf Yahya dakika ya 75.

Kwa upande wa timu ya Super Eagle ambayo ni kipigo chake cha pili mfululizo baada ya mchezo wa kwanza kufungwa kwa idadi kama hiyo ya mabao na Spirit, bao lake la kufutia machozi lilifungwa na mchezaji wake Jabir Ali dakika ya 26.

Nayo timu ya Spirit ambayo ilishuka katika dimba la Mao Zedong B saa 10:00 iliifunga Chumbuni mabao 2-0 ambayo yalifungwa na Talib Mtumwa Suleiman dakika ya 68 na Hamad Juma Isi-haka dakika ya 90.

Mbali ya  michezo hiyo lakini pia katika uwanja wa Mao Zedong A saa 10:00 kulikuwa na mchezo kati ya Mwembe Makumbi na Jamaica ambao ulimalizika kwa wanaume hao kutoka sare ya kutofungana.