NA MAULID YUSSUF,
WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Riziki Pembe Juma, amesema Wizara hiyo inaendelea kufanya bidii kuhakikisha inazalisha Walimu wazalendo wa masomo ya Sayansi nchini, ili kupata wataalamu wazuri wa baadae.
Akizungumza wakati wa hafla ya kumpongeza Mwalimu wa Somo la hesabati kutoka Skuli ya FEZA ukumbi wa Wizara ya Elimu Mazizini mjini Unguja, amesema kuwa jitihada ya kusomesha Wanafunzi masomo ya sayansi kwa bidii pia kutasaidia sana kupata Walimu wa masomo hayo wa baadae.
Riziki amewataka Walimu wa Skuli ya FEZA kuandaa mikutano maalum na Walimu wa Skuli nyengine ili kubadilishana mawazo yatakayoleta mabadiliko chanya katika Skuli zote za Zanzibar hasa ya ufaulu wa juu kwa masomo ya Sayansi.
Nae Naibu Katibu Mkuu Utawala na Uendeshaji wa Wizara ya Elimu, Mwalimu Abdullah Mzee Abdullah amesema mashirikiano mazuri baina ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar na Skuli binafsi ni miongoni mwa mafanikio makubwa katika kuendeleza sekta ya Elimu nchini.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Feza Bwana Ali Nughu amesema ili kuzidisha ari ya kusomesha kuna umuhimu kwa Walimu wanaofanya vizuri katika masomo yao kupewa zawadi ili nao wahamasike katika kutafuta mbinu mbadala za kusomeshea.