NA ASYA HASSAN

TAASISI ya Panje Project imeiomba serikali kuanzisha mfuko maalum kwa ajili ya kuiwezesha taasisi hiyo kutoa mafunzo kwa jamii juu ya usalama majini.

Akizungumza katika mafunzo ya usalama kwenye maji kwa Watu wenye ulemavu, Mratibu wa taasisi hiyo Abasi Ramadhani Makame, alisema hatua hiyo itawawezesha kuifikia jamii na taasisi mbalimbali za serikali kwa ajili ya kuwapatia mafunzo hayo.

Alisema Zanzibar ni nchi iliyozungukwa na bahari hali inayopelekea kutokea ajali za mara kwa mara hivyo kuwepo kwa mfuko huo kutasaidia kuokoa maisha ya walio wengi hasa kwa watumiaji wa bahari wakiwemo wasafiri, wavuvi, wanaoogelea pamoja na wakulima wa mwani.

“Lengo la taasisi yetu ni kuona wananchi wote wanakuwa na uelewa juu ya kujikinga na kujiokoa na majanga mbalimbali pale yanapotokezea,” alisema.

Akizungumzia vyombo vya usafiri wa baharini, alisema ni vyema kuweka utaratibu maalum  wa kuwapa vifaa vya uokozi na kuvaa kabla ya kuanza safari ili kuimarisha usalama kwa wasafiri hao.

Alifahamisha kwamba wameamua kutoa mafunzo kwa makundi hayo maalumu kwani nao wana haki ya kupatiwa taaluma na huduma mbalimbali kama walivyo watu wengine.

Kwa upande wake mwalimu wa taasisi hiyo Muhamadi Idrisa Simai, alisema wanatoa elimu hiyo ili kuisaidia jamii kutambua athari zilizopo ndani ya maeneo ya maji na kuchukua tahadhari kwa lengo la kujilinda wenyewe na wenzao pale kunapotokezea maafa yatokanayo na maji.

Kwa upande wa washiriki hao walisema mafunzo hayo yamewasaidia kujuwa jinsi ya kujikinga na maafa wakiwa katika maji.

Aidha wameiomba taasisi hiyo kuendelea kuwapatia mafunzo hayo mara kwa mara ili wazidi kujenga uelewa juu ya masuala hayo ambapo hivyo wameahidi kwenda kuwafikishia wenzao taaluma hiyo ambayo wameipata.

Taasisi hiyo imeanzishwa mwaka 2013 na imekuwa ikitoa mafunzo ya usalama kwenye maeneo ya maji kwa makundi mbalimbali kwa lengo la kuiweka nchi kwenye usalama juu ya majanga yanayotokana na maji.