NA ABOUD MAHMOUD

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kupitia Wizara husika imeshauriwa kuendeleza mashirikiano baina yao na wasanii wa fani ya uchoraji, ili waweze kuitangaza nchi kitaifa na kimataifa.

Kauli hiyo imetolewa na meneja wa hoteli ya Emerson, Lisenka Beetstra wakati alipokuwa akifungua maonyesho ya picha zilizochorwa na wasanii wa Zanzibar yanayofanyika katika hoteli hiyo Hurumzi.

Alisema wasanii wa uchoraji wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kutangaza utalii wa Zanzibar kupitia picha wanazochora na watalii kuzinunua.

“Naiomba Serikali yetu iendelee kuwa bega kwa bega na wasanii wetu hawa ambao  bado wapo katika safari ya kutafuta maisha yao yawe mazuri, naamini kama serikali itaendelea kutoa mashirikiano  Zanzibar itazidi kutambulika kimataifa kupitia fani hii,”alisema .

Lisenka alieleza kwamba wachoraji wa Zanzibar endapo wataendelezwa wanaweza kufika mbali kwa kupata uelewa  zaidi wa kuchora picha zinazohitajika katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia.

Aidha meneja huyo aliwashauri wachoraji wa Zanzibar wasivunjike moyo na waendelee kujituma ili waweze kufika mbali na kutatua changamoto walizonazo.