NA HAFSA GOLO

WANANCHI wamepongeza uamuzi wa serikali ya awamu ya saba inayoongozwa na Dk. Ali Mohamed Shein wa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ukiwemo wa ujenzi wa nyumba za makazi na majengo ya biashara.

Wakizungumza na Zanzibar Leo, walisema hatua hiyo mbali ya kuleta mabadiliko ya haiba ya mji wa Zanzibar, pia itaongeza umaarufu wa Zanzibar na kuifanya kuwa kitovu cha biashara.

Wakizungumza katika hafla ya ufunguzi wa jengo la biashara la Sheikh Thabit Kombo lililopo Michenzani,walisema mradi huo utaongeza kasi ya ukuaji uchumi.

Zaina Rashid alisema Dk. Shein ni kiongozi mwenye fikra sahihi na mtazamo mpana katika kuibadilisha Zanzibar ili iendane na ulimwengu wa sayansi na teknolojia.

Ali Hassan wa  Kwahani alisema serikali inaendelea kutekeleza kwa vitendo azma ya muasisi wa Mapinduzi ya mwaka 1964, mzee Abein Amani Karume.

“Kwa kweli kasi ya maendeleo inayosimamiwa na Dk. Shein imedhihirisha wazi utekelezaji wa vitendo wa fikra za mzee Karume, ambae alipambana kwa kila hali kuibadilisha Zanzibar katika kipindi kifupi cha uhai wake,” alisema.