NA SALUM VUAI

WIZARA ya Nchi (OR) Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, imeeleza kuridhishwa na kiwango cha barabara ya Mambosasa/Mwera Wilayani iliyojengwa kwa lami na kampuni ya MECCO ya Tanzania.

Akikagua barabara hiyo jana baada ya kukamilika kazi ya kutandika lami, waziri wa wizara hiyo Haji Omar Kheri, alisema ni faraja kwamba ujenzi huo umemalizika kabla Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein hajamaliza muda wake wa uongozi.

Alifahamisha kuwa, Dk. Shein ndiye aliyeagiza barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 3.4 ijengwe kwa lami ili kuwaondoshea wananchi usumbufu wa usafiri.

Waziri huyo aliipongeza kampuni ya MECCO kwa kuifanya kazi hiyo kwa mujibu wa kiwango kilichotarajiwa, akisema hatua hiyo inaongeza imani ya serikali kwa wakandarasi wazalendo.

“Ingawa kulikuwa na changamoto ndogondogo zinazotuhusu sisi (serikali) na nyengine kwa mkandarasi, lakini wamejitahidi kuhakikisha wanaimaliza na kuikabidhi kwetu,” alisema.    

Alihimiza kukamilishwa kwa kazi ndogondogo zilizobakia ikiwemo misingi ya kupitishia maji pamoja na kuwekwa alama za barabarani ili kuepusha ajali zisizokuwa za lazima.

Kwa upande mwengine, alitoa wito kwa madereva wa gari za mizigo kufuata masharti kwa kutopitisha gari zenye uzito unaozidi tani 10 na kwamba atakayeshikwa akifanya hivyo ajiandae kukabiliana na adhabu.

Aidha, alisema suala la kuwajengea wananchi barabara za kisasa limo katika ilani ya uchaguzi ya CCM 2010-2020, ili waweze kuendesha shughuli zao za kiuchumi, biashara na kijamii na kutokomeza umasikini.

Mapema akitoa maelezo kuhusu ujenzi huo, Mhandisi mkuu wa wizara hiyo Ali Omar, alisema shilingi 3,500,000,000 zimetumika kujenga barabara hiyo na zote zimetolewa na serikali.