LONDON, England
MANCHESTER UNITED kwa sasa haina mpango wa kusaini beki mpya wa kati msimu huu wa joto, licha ya safu ya ulinzi kuonyesha udhaifu katika mchezo wa kwanza wa ligi kuu dhidi ya Crystal Palace.
Mashetani wekundu hao hawakuwa na kiwango kizuri kwenye uwanja wa Old Trafford Jumamosi walipopoteza kwa mabao 3-1, huku Victor Lindelof akiwaonyesha udhaifu mkubwa dhidi ya Wilfried Zaha.
Kiwango kibovu kilichoonyeshwa na United chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer, kumezua lawama nyingi kwa wachezaji wa zamani wa timu hiyo, akiwemo Gary Neville ambaye alidai timu hiyo haiwezi kutwaa taji kama hawatasajili beki wa kati.
Lakini, kwa mujibu wa ‘The Athletic’, United haitaangalia mapungufu ya beki wa kati kabla ya dirisha kufungwa na wataendelea kuangalia maeneo mengine.
Ole Gunnar Solskjaer ambaye alikataa kumlaumu Lindelof kutoka na kipigo hicho na kubainisha kuwa tayari ana mabeki wa kutosha wa kati na hana haja tena ya kusajili.
Eric Bailly alikuwa kwenye benchi wakati Timothy Fosu-Mensah, ambaye alicheza beki wa kulia dhidi ya Palace, pia anaweza kucheza katikati. Axel Tuanzebe bado anaendelea kufanya mazoezi kamili , wakati Phil Jones bado ni sehemu ya kikosi na Teden Mengi amekuwa akifanya mazoezi na kikosi cha kwanza.