NAIROBI, KENYA

JAJI mkuu nchini Kenya David Maraga amemtaka rais Uhuru Kenyatta kulivunja bunge kwa sababu halina wabunge wanawake wa kutosha.

Katika barua kwa rais Kenyatta,jaji huyo alisema kwamba kushindwa kuwa na wabunge wengi wa kike ni ukiukaji wa katiba na ubaguzi dhidi ya wanawake.

Katiba inasema kwamba jinsia moja haiwezi kudhibiti zaidi ya thuluthi mbili ya viti vya bunge.

Hata hivyo wanawake wana viti vichache ikilinganishwa na viti 116 vinavyohitajika katika bunge hilo la wabunge 350.

”Bunge limefeli ama kupuuza sheria zinazohitajika kuidhinisha sheria hiyo ya jinsia,licha ya maagizo manne ya mahakama”,alisema jaji Maraga.

Alisema kisheria alitarajiwa kumshauri rais kulivunja bunge.

Spika wa bunge Justin Muturi alisema kwamba kuvunjwa kwa bunge ni chaguo lisilowezekana.

Katiba mpya ya Kenya ilizinduliwa 2010, na sheria ya jinsia kuhusu thuluthi mbili ilifaa kuidhinishwa baada ya miaka mitano.

Huku kukiwa kumekuwa na mjadala kuhusu suala hilo, bunge hilo lenye wanaume wengi halijapata mbinu ya kupata wanawake wengi bungeni , huku baadhi ya wabunge hao wakihoji dhidi ya kubuni viti vingi hususan vya wanawake na badala yake kuwataka wanawake kuingia katika kinyang’anyiro cha kuwania ubunge mashinani.

”Hatuwezi kusahau kuhusu changamoto zinazotukabili tunapojaribu kuidhinisha suala hili na kuligeuza bunge kuwa eneo la kupigana kutokana na jinsia”,alisema katika taarifa yake.

Jaji Maraga alisema kwamba bunge la kumi halikuwa na muda wa kutosha kuidhinisha sheria inayohitajika kuhalalisha sheria hiyo ya jinsia.

Kulingana na Maraga,Mahakama ya upeo chini ya aliyekuwa jaji mkuu Willy Mutunga aliagiza bunge kuidhinisha sheria hiyo kufikia tarehe 27 Agosti 2015.

Jaji huyo alisema kwamba pingamizi kadhaa ziliwasilishwa mahakamani zikilitaka bunge kuidhinisha sheria hiyo.

Hata hivyo Bunge lilishindwa kuidhinisha miswada iliowasilishwa mbele yake.

Maraga aliongezea kwamba sheria hiyo ya jinsia inazuia aina yoyote ya ubaguzi katika uteuzi na uchaguzi nchini kulingana na jinsia.

Wanawake na wanaume wana haki ya fursa sawa , kiuchumi, kitamaduni na kijamii.