COLOMBO,SRI LANKA

SRI LANKA imezirejesha nchini Uingereza kontena zilizokuwa zimebeba takataka hatari huku Serikali ya Colombo ikisema kuwa ziliingizwa nchini humo kwa kukiuka sheria za kimataifa zinazosimamia usafirishaji wa mada hatarishi.

Maofisa wa forodha wa Sri Lanka walieleza kuwa,kontena hizo 21 zenye tani za takataka zisizopungua 260, ziliwasili katika bandari kuu ya mji mkuu Colombo kati ya Septemba mwaka 2017 na Machi 2018 na kwamba juzi Jumamosi zilisafirishwa kuelekea nchini Uingereza.

Ofisa wa forodha wa Sri Lanka alieleza kuwa kontena hizo kutoka Uingereza zilipasa kuwa na vitu kama magodoro yaliyotumiwa na mazulia,hata hivyo ndani ya kontena hizo kumepatikana takataka za hospitalini.

Sri Lanka ilizirejesha nchini Uingereza kontena zilizokuwa zimebeba takataka hatari huku Serikali ya Colombo ikisema kuwa ziliingizwa nchini humo kwa kukiuka sheria za kimataifa zinazosimamia usafirishaji wa mada hatarishi.

Msemaji wa Idara ya Forodha katika bandari ya Colombo Sri Lanka,Sunil Jayaratne alisema kuwa muhusika wa mzigo huo alikiri kupokea kontena 21 na kwamba sasa wanashughulikia kudai fidia kutoka kwa waliohusika na kuingizwa nchini humo kontena hizo zenye takataka hatarishi.

Maofisa wa forodha wa Colombo walipohojiwa ili wataje ni aina gani ya takataka za hospitalini zilizokutwa ndani ya kontena hizo kutoka Uingereza walisema kuwa zilikuwa na mazulia,bandeji na viungo vya binadamu kutoka mochwari.

Wakati huo huo ilielezwa kuwa kontena nyengine kutoka Uingereza zipatazo 242 ambazo Serikali ya Colombo ilisema zimepakia takataka hatarishi zimetelekezwa katika bandari hiyo na katika eneo huru la biashara nje ya mji wa Colombo.

Katika miaka ya karibuni nchi za Asia zilikataa kutumiwa katika jalala la kutupia taka za nchi tajiri duniani na zimekuwa zikirejesha taka hizo katika nchi zilipotokea.