MOSCOW,URUSI

URUSI  imesema nchi za magharibi hazipaswi kufanya pupa ya kuihukumu juu ya kutiliwa sumu mpinzani wa Serikali ya nchi hiyo Alexei Navalny wakati ambapo mazungumzo katika nchi za magharibi juu ya kuiadhibu Urusi yanapamba moto.

Urusi ilitoa kauli hiyo siku moja baada ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kusema kuwa kuna jaribio la kumuua Navalny kwa kumtilia sumu aina ya Novichok ya tokea enzi za kisovieti inayoathiri mishipa ya fahamu.

Merkel alisema atawasiliana na washirika wa NATO kujadili hatua watakazochukua kujibu kitendo cha Urusi.

Umoja wa Ulaya ulisema unaweza kuweka vikwazo dhidi ya Urusi.

Muungano wa kijeshi wa NATO uliitisha kikao cha haraka kujadili uchunguzi wa madaktari wa Ujerumani uliothibitisha kwamba Navalny alitiliwa sumu madai ambayo Urusi iliyakanusha.