NA MWANTANGA AME

MGOMBEA wa Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama cha ADA TADEA, Juma Ali Khatib, amesema akichaguliwa kuwa rais ataendeleza miradi mikubwa ya kimkakati inayolenga kukuza uchumi na kuongeza ajira kwa vijana.

Khatib alisema hayo wakati akizindua kampeni za chama chake katika uwanja wa Sogea Magaeni, mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.

Alisema ataendeleza na kuimaliza miradi yote muhimu ambayo imesimamiwa na Rais Dk. Ali Mohamed Shein, ili kuunga mkono kazi nzuri aliyoifanya katika kipindi cha miaka kumi ya uongozi wake.

“Nikichaguliwa na kuwa Rais wa Zanzibar, azma yangu ni kutekeleza miradi ya kimkakati iliyoanzishwa na serikali ya awamu ya saba ukiwemo ujenzi wa bandari ya Mpigaduri Maruhubi, nitajenga uwanja wa ndege wa Karume ili kuruhusu ndege kubwa kutua na kuongeza idadi ya watalii,” alisema.

Khatib ambaye pia ni Waziri asiye na Wizara maalumu, alimshukuru Dk. Shein kwa kujumuisha viongozi wa vyama vya upinzani katika serikali yake jambo lililomsaidia kupata uzoefu wa hali ya juu wa uongozi.

Aidha, alisema akichaguliwa anakusudia kufufua eneo la viwanda vidogo vidogo lililopo Amani kwa ajili ya kuzalisha ajira nyingi Zaidi kwa vijana na kurudisha enzi ya Zanzibar ya kupiga hatua kubwa katika sekta hiyo.

Kwa mfano alisema katika miaka ya 1980, Zanzibar ilikuwa maarufu kwa kuwa na viwanda vingi vidogo vidogo vya aina mbali mbali ikiwemo masufuria, sabuni, waya za umeme pamoja na mafuta ya nazi na kusafirisha nje ya nchi.

”Mimi nilibahatika kufanya kazi katika Shirika la viwanda vidogo vidogo, tulikuwa tukizalisha bidhaa mbali mbali na kuifanya Zanzibar kusafirisha nje ya nchi,”alisema.

Mapema mgombea mwenza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya ADA TADEA, Hassan Kijogoo, alisema wanakusudia kuifanya Zanzibar kuwa lango kuu la uchumi kwa kusafirisha bidhaa mbalimbali hadi katika visiwa vya Comoro.

”Tukichaguliwa mimi na mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa chama chetu, John Shibuda tunakusudia kuifungua Zanzibar na kuwa lango kuu la kiuchumi kwa kutumia fursa zilizopo kwa nchi jirani ikiwemo Ngazija (Comoro) na Kenya,”alisema.