NA MWANDISHI WETU

CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA, ZNZ), kimepongeza ushirikiano uliooneshwa na jamii kwa jeshi la polisi mkoa wa Kusini Unguja uliowezesha kutiwa mikononi matuhumiwa wa mauaji.

Hivi karibuni jeshi hilo katika mkoa wa Kusini Unguja limethibitisha kumtia mbaroni Haji Jaha Issa (25) mkaazi wa Paje wilaya ya Kusini Unguja ambaye anatuhumiwa kuhusika na kifo cha Hajra Abdallah Abdallah (21).

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa chama hicho hapa Zanzibar, Dk. Mzuri Issa alisema jamii ikiendelea kuondosha muhali kwa kuwafichua wahalifu wa matukio mbalimbali upo uwezekano wa kukomeshwa vitendo vya ukatili na udhalilishaji.

Mkurugenzi huyo aliviomba vyombo vya kusimamia sheria kuhakikisha wanatenda haki dhidi ya tukio hilo ili kustawisha utawala wa sheria na kukomesha vitendo hivi vya kudhuru wanawake kutokana na udhaifu wao wa kimaumbile.

Chama hicho kimerikodi matukio 17 ya mauaji ya wanawake Zanzibar tangu mwaka 2016 ambapo kati ya matukio hayo, ni kesi nne ikiwemo ya marehemu Hajra ndizo zilizofikishwa mahakamani.

Kesi nyengine tatu zilizofikishwa mahakamani inawahusu Wasila Mussa (21), Samira Sultan (56) na Zawadi Paulo (35) ambazo zote zinaendelea katika mahakama kuu iliyopo Vuga mjini Zanzibar.

Kwa mujibu wa kamanda wa Polisi Mkoa huo, Suleiman Hassan Suleiman alisema jeshi la polisi limefanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo mwanzoni mwa mwezi uliopita katika kijiji cha Msisi wilaya ya Handeni Mkoani Tanga.

Kamanda Suleiman alisema kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kumetokana na raia wema kutoa taarifa baada ya mtuhumiwa kuwaomba hifadhi ili aendelee kujificha kwa kukwepa mkono wa sheria.

Kamanda huyo alisema jeshi lake baada ya kupata taarifa hizo lilifika eneo hilo na kumkata kumrudisha Zanzibar sambamba na kumfikisha mahakamani kwa ajili ya kukabiliana na tuhuma zinazomkabili.

“Kazi ya kutafuta na kukamata inakua nyepesi kwa jeshi la polisi pale ambapo jamii itatoa ushirikiano, raia wema walitupa taarifa kama mtuhumiwa yuko Tanga kijijini eneo la Msisi Handeni, anaomba hifadhi”, alisema.