NA ASIA HASSAN
CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA, ZNZ) kimewaomba wazazi na walezi kuacha tabia ya kuficha matukio ya udhalilishaji wanayofanyiwa watoto ndani ya jamii.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na chama hicho kwa vyombo vya habari ilisema kuwepo kwa wazazi na walezi wenye tabia ya kuficha matukio hayo, baada ya mtoto kubakwa au kulawitiwa ni kuathiri kasi kubwa ya maendeleo ya wanawake na mipango ya nchi katika kupambana na vitendo vya udhalilishaji hapa nchini.
Alifahamisha kwamba hivi karibuni mtandao wa kupambana na ukatili wa kinjisia kwa wanawake na watoto Wilaya ya Mkoani Pemba, ulipokea taarifa kwamba mtu mmoja anadaiwa kuwabaka watoto watatu, ambapo kati yao wawili wakiwa na umri wa miaka tano (5) na mmoja mwenye umri wa miaka sita (6).
Alisema mtu huyo aliyefahamika kwa jina la Salmini Musa Juma (29) mkaazi wa Jombwe shehia ya Muambe Wilaya ya mkoani, Kusini Pemba, anadaiwa kufanya tukio hilo Agosti 25 katika Shehia hiyo.
Taarifa hiyo ilieleza kwamba mratibu wa TAMWA Zanzibar kwa upande wa Pemba, Fat-hiya Mussa Said, alisema wamepokea taarifa hiyo kutoka mtandao huo kwamba kati ya matukio ya kuwadhalilisha watoto watatu ni mawili tu ndio yameripotiwa katika kituo cha polisi Kengeja, Mkoa wa Kusini Pemba.
Mratibu huyo alifahamisha kwamba mtandao unaendelea kuwashawishi wanafamilia hao waondoe muhali na kuchukua hatua ya kuripoti tukio hilo katika vyombo vya sheria, ili mfanyaji aweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
Aidha alifahamisha kwamba kwa mujibu wa taarifa kutoka jeshi la Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba, ilisema kwamba mtuhumiwa wa matukio hayo anakabiliwa na makosa mawili kosa la shambulio la aibu na kumwingilia kinyume na maumbile mtoto wa kike.