NA MWINYIMVUA NZUKWI

IMEELEZWA kuwa mpango wa kunusuru kaya maskini unaosimamiwa na Mfuko wa maendeleo ya jamii Tanzania (TASAF) umechangia kuongeza kasi ya ukuaji uchumi wa kaya na kupunguza utegemezi.

Akiwasilisha matokeo ya utafiti juu ya dhana na uhalisia kuhusu ruzuku kwa walengwa wa mpango huo katika kikao kazi kwa wahariri wa vyombo vya habari, Mtaalamu wa tathmini na ufuatiliaji Fariji Mishael alisema utafiti umebaini kaya za walengwa zimepunguza kufanya vibarua badala yake zinafanya shughuli binafsi za kaya.

Alisema kutokana na ruzuku inayotolewa, kaya zimeanzisha miradi mbali mbali ya kiuchumi na kuwa na nafasi kubwa ya kumiliki mifugo, kulima mashamba yao na kujiwekea akiba.

“Matokeo haya yanapingana na dhana mbali mbali ikiwemo ya kwamba ruzuku itawafanya walengwa kuwa wavivu na tegemezi, lakini utafiti umekuja kubaini tofauti,” alisema Mishael.

Aliongeza kuwa kutokana na ruzuku inayotolewa kwa kaya, imechochea matumizi ya kaya katika chakula badala ya matumizi kwenye uvutaji wa sigara na kunywa pombe.

Aliongeza kuwa uandikishaji wa watoto skuli na kiwango cha ufaulu kimeongezeka sambamba na kuongezeka kwa mahudhurio ya kliniki kwa watoto chini ya miaka mitano na mama wajawazito.

“Hali hii imechangia kaya za walengwa kujiunga na mpango wa bima ya afya mara tatu zaidi ya kaya zisizo za walengwa na kwamba kwa kila shilingi inayolipwa inazalisha kati ya shilingi 1.5 hadi 2.5 zinazoingia katika uchumi wa maeneo husika,” aliongeza.

Aidha alieleza kuwa hakuna uhusiano wowote kati ya ongezeko la watoto waliozaliwa kwenye kaya maskini na utoaji wa ruzuku kwa walengwa na kupinga dhana kuwa mpango huo unachochea ongezeko la watoto.

Hata hivyo, alieleza kuwa serikali inatumia asilimia 0.4 ya mapato yake kugharamia kaya milioni moja za walengwa kiwango ambacho ni kidogo ikilinganishwa na viwango vinavyotolewa katika nchi nyengine za kusini mwa jangwa la Sahara.