NA MWAJUMA JUMA

CHAMA Cha mpira wa Wavu Tanzania (TAVA),  kupitia kamisheni yake ya waamuzi inatarajia kuendesha mafunzo ya awali ya ndani na ya kitaifa.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kufanyika Septemba 28 hadi Octoba 3 jijini Dar es Salaam na wale ambao watataka kushikiriki wanatakiwa kufika katika kituo cha Mafunzo siku moja kabla ya Mafunzo.

Kwa mujibu wa barua ya chama hicho iliyotumwa kwa chama cha mchezo huo Zanzibar (ZAVA), mafunzo yatawahusisha waamuzi pekee wenye sifa na ndio ambao wataruhusiwa kuendesha mashindano yoyote ya mpira huo nchini.

Hata hivyo barua hiyo ambayo ilisainiwa na  Alfred Selengia Katibu wa TAVA ilisema mafunzo hayo yana lengo la  kuimarisha fani ya uwamuzi kwa waamuzi wapya na wale ambao walipata kozi ya awali mwaka 2017.

“Ifahamike kwamba waamuzi pekee wenye sifa ndio watakaoruhusiwa kupewa nafasi ya kuendesha mashindano yoyote ya mpira wa wavu nchini”, alisema Selengia.