NA MWANAJUMA MMANGA

JESHI la Polisi Mkoa wa Kusini Unguja, limekamata mapipa saba na  madumu 12 ya pombe za kienyeji (Tende) ikiwa na ujazo wa lita 20 kila moja huko Kiboje Wilaya ya Kati Unguja.

Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Suleiman Hassan Suleiman, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo huko Kiboje Kinooni, Septemba 23 mwaka huu majira ya saa 8:30 mchana huko Kiboje Wilaya ya kati mkoa huo.

Alisema ulevi huo, wameukamata baada ya kuwakuta kinamama wakiwa jikoni wakipika pombe hiyo na kutimua mbio na pasipojulikana na kufanikiwa kuukamata ulevi huo na mwengine uliokuwa umerowekwa katika mapipa  na kuumwaga.

Suleiman, alisema kuwa juhudi ya kukamata ulevi huo baada ya kufanya operesheni maalum kwa wanaofanya biashara za dawa za kulevya, wasambazaji na wahalifu katika maeneo mbali mbali ya mkoa huo.

Hivyo, aliwataka wananchi kuendelea kutoa mashirikiano ya karibu na jeshi la polisi ili kuwafichua wale wenye tabia kama hiyo na kuchukuliwa hatua za kisheria dhidi yao na kuachana na biashra kama hizo na badala yake kujishughulisha na kazi za halali ambazo zitaweza kujipatia kipato ili kujikimu kimaisha.