NA HAFSA GOLO
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Zanzibar, imesema kuna uwezekano wa kufikiwa lengo la ukusanyaji mapato baada ya ongezeka la mapato ya kodi nyengine katika miezi miwili ya mwanzo wa mwaka wa fedha 2020/2021.
Matumaini hayo yanatokana na taasisi hiyo kukusanya shilingi bilioni 39.68 katika mwezi wa Julai na Agosti mwaka huu.
Ofisa msimamizi wa kodi wa mamlaka hiyo, Abdallah Seif Abdallah alieleza hayo alipokua akizungumza na mwandishi wa gazeti hili ofisini kwake Mlandege, mjini Unguja.
Alisema TRA imeona dalili nzuri za kuongezeka kwa makusanyo katika mwezi wa Agosti unaochangiwa na kuongezeka kwa watalii wanaoingia nchini.
“Meli za biashara na mizigo zimeanza kuingia Zanzibar kutoka maeneo tofauti ulimwenguni kama vile Dubai, China na India hali ambayo itaongeza shughuli za kibiashara”, aliongeza ofisa huyo.
Mbali na hilo, alisema mikakati mengine itakayotekelezwa ndani ya mamlaka hiyo ni kufanya ukaguzi kwa mashirika ya umma na kwenye biashara nyengine kama vile bidhaa za mchele na sukari ili kuhakikisha hakuna ukwepaji kodi.
“Mkakati huo utakwenda sambamba na zoezi la kuwakagua mara kwa mara walipa kodi wa kawaida pamoja na sekta za ujenzi ili kuhakikisha kodi inalipwa kwa mujibu wa sheria,” alieleza.
Aliwaomba wananchi na wafanyabiashara kuendelea kulipa kodi kwa wakati na kuwa wazalendo wa nchi yao kwani nchi hujengwa na wananchi kupitia vyanzo mbali mbali ikiwemo kodi.
Alifahamisha kwamba TRA imeanzisha mfumo wa ulipaji kodi kwa njia za elektroniki kurahisisha utumaji wa taarifa na ulipaji kodi bila ya mteja kufika katika ofisi za mamlaka hiyo.