WASHINGTON, MAREKANI

RAIS Donald Trump wa Marekani amemtangaza mhafidhina na jaji wa jimbo la Indiana Amy Coney Barrett kuziba pengo lililoachwa na jaji Ruth Bader Ginsburg katika Mahakama ya juu nchini humo.

Jaji Gisburg alifariki dunia Septemba 18. Hatua hiyo inayotarajiwa kuungwa mkono na maseneta wa Republican inafungua njia kwa wahafidhina wengi zaidi kwenye mahakama hiyo ya juu.

Barrett, karani wa jaji wa zamani wa marehemu jaji Antoni Scalia alisema baada ya uteuzi huo kwamba anaipenda Marekani pamoja na katiba yake na kuongeza kuwa jaji anatakiwa kuitumia sheria kama ilivyoandikwa na kwamba majaji si watunga sera.

Trump aliwaambia waandishi wa habari kwamba anataraji jaji Barrett atathibitishwa kwenye mahakama hiyo kabla ya uchaguzi wa Novemba 3.