WASHINGTON, MAREKANI

AKIWA anajipanga kwa ajili ya mdahalo wake wa kwanza kabla ya uchaguzi wa Novemba,Rais Donald Trump wa Marekani anakabiliwa na tuhuma mpya za kulipia kodi kidogo ama kutolipia kabisa kwa miaka kadhaa kabla hajaingia madarakani.

Gazeti la New York Times liliibuwa nyaraka zinazoonesha kuwa rais huyo bilionea alilipia dola 750 tu za kodi ya mapato katika mwaka 2016, mwaka alioingia madarakani,na hakulipa kodi yoyote kwa miaka kumi kati ya 15 kabla ya hapo,kwani alidai kupoteza fedha nyingi zaidi kuliko alizokuwa akiingiza kwenye biashara zake.

Trump, ambaye alizikanusha taarifa hizo akisema ni za uzushi, anajitayarisha kwa mdahalo wa ana kwa ana unaofanyika,kati yake na mgombea wa Democratic,Joe Biden.

Kiongozi huyo wa Republican alivunja mila ya muda mrefu ya marais kuchapisha marejesho yao ya kodi, akiwa alifungua kesi nyingi mahakamani kuzuwia uchapishwaji huo,hali inayochochea uvumi juu ya kile kilichomo ndani yake.