ULIMWENGU mzima kwa sababu tofauti unaufuatilia kwa karibu sana uchaguzi mkuu nchini Marekani ambao umepangwa kufanyika Novemba 3 mwaka huu.

Uchaguzi huo unaovutia hisia unafuatiliwa kwa sababu mbalimbali ambapo mataifa yenye ushindani wa karibu na Marekani pengine wangeomba aingie madarakani mpinzi Joe Biden kutokana na kubanwa na sera za Trump.

Nchi masikini kama za huku kwetu ambazo zinaambiliwa kuwa hazina demokrasia ya watu wa magharibi, zinafuatilia uchaguzi ili kujifunza ukomavu wa kidemokrasia.

Pamoja na sababu hizo, uchaguzi wa Marekani pia unafuatiliwa kutoka na kaliba ya wagombea akiwemo rais wa sasa anayewania nafasi hiyo kwa mara ya pili Donald Trump na mpinzani wake Joe Biden.

Viongozi hao wanaowania madaraka wamekuwa na upinzani mkubwa kiasi cha kauli zao wanazozitoa katika kupinga ama kuunga mkono hoja zinasababisha   msisimko mkubwa.

Hata hivyo kauli za Trump ndizo zinazoonekana kuwa na utata kiasi cha wakati mwengine wetu wengi kumshangaa kiongozi mkubwa kama huyo anawezaje kutoa kauli za namna hiyo.

Kwa mfano hivi karibuni rais huyo alitoa kauli akisema kuwa hayupo tayari kuachilia madaraka kwa amani. Kauli ya namna hii hatujaizoea kuisikia ikitolewa na kiongozi anayetoka katika taifa linalojiita kuwa limestaarabika na la kidemokrasia kama Marekani.

Hii si mara ya kwanza kwa Trump kutoa kauli ya kupinga matokeo ya uchaguzi kwani mnamo mwaka 2016, alikataa kukubali matokeo ya uchaguzi katika kinyang’anyiro kati yake na mgombea wa democratic, Hillary Clinton, hatua ambayo alitajwa kama shambulio dhidi ya demokrasia ya Marekani.

Kura inayopigwa kwa posta inaweza kuibiwa? Idadi ya kura zitakazopigwa kupitia njia ya posta zinatarajiwa kuongezeka katika uchaguzi wa mwaka huu nchini Marekani kutokana na hofu ya maambukizi ya virusi vya corona.

Lakini Ellen Weintraub, kamishena wa Tume ya Uchaguzi, alisema hakuna msingi wowote wa kufanyika kwa udanganyifu ama njama ya kuiba kura endapo zitapigwa kwa mfumo wa posta.

Kumekuwa na visa vichache vya udanganyifu katika mfumo wa upigaji kura kwa njia ya posta, kwa mfano katika uchaguzi wa mchujo wa mwaka 2018 North Carolina, ambapo uchaguzi ulirudiwa tena baada ya kubainika mgombea wa Republican aliingilia mchakato wa upigaji kura.

Pia kulikuwa na kisa kingine mwaka huu New Jersey ambapo madiwani wawili wa Democratic walishitakiwa kwa kuhusika na udanganyifu uliohusisha upigaji kura kupitia posta.

Lakini kiwango cha udanganyifu katika mchakato wa uchaguzi wa Marekani uko chini sana kati ya asilimia 0.00004 na 0.0009, kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2017 uliofanywa na Kituo cha Haki cha Brennan.

Hata hivyo Trump ameonesha shaka ya kukubaliana na matokeo kwenye uchaguzi mkuu kwa sababu anaonekana kupinga na kutokuwa na imani na mfumo wa upigaji kura kwa kutumia njia ya posta.

Akizungumza na waandishi wa habari ikulu jijini Washington hivi karibuni, Trump alisema, “Napinga vikali upigaji kura kwa njia ya posta, upigaji kura wa namna hiyo ni majanga”.

Mwanahabari alipo mkatiza na kumwambia kwamba watu wanaandamana, Trump alijibu, “Futilieni mbali uchaguzi na kutakuwa – na amani – hakutakuwa na suala la kupokezana madaraka, kwa kweli, kutakuwa na muendelezo”, alisema.

Trump alisema anaamini matokeo ya uchaguzi huenda yakaamuliwa katika mahakama ya juu, huku majimbo zaidi yanatoa wito wa upigaji kura kwa njia ya posta, yakisisitiza umuhimu wa wapiga kura kuwa salama dhidi ya maambukizi ya corona.

Katika hatua nyengine spika wa democratic bungeni Nancy Pelosi, ambaye ni mwanasiasa wa tatu mwenye ushawishi mkubwa zaidi Washington, aliwaambia wanahabari siku kwamba hakushangazwa na tamko la Trump.

Pelosi aliongeza kuwa rais anapenda watu wanaojitakia makuu kupitia jukumu lao serekalini, akitoa mfano wa Vladimir Putin wa Urusi, Kim Jong-un wa Korea Kaskazini na Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki.

“Lakini namkumbusha, wewe sio Korea Kaskazini, wewe sio Uturuki wala Urusi, Trump…. Kwa nini usijaribu angalau kuheshimu kiapo cha ofisi yako”, alisema Pelosi.

Akizungumza na wanahabari Katika eneo la Delaware, mgombe wa urais mpizani wa Trump, Joe Biden alisema kwamba matamshi ya Trump ya kukataa upigaji kura kwa mfumo wa posta hayana mantiki.

Biden mwenyewe amelaumiwa na wahafidhina kwa kuchochea vurugu katika uchaguzi aliposema mwezi Augosti kwamba kuna mtu anaamini hakutakuwa na vurugu nchini Marekani ikiwa Donald Trump atachaguliwa?”

Mwezi uliopita, Clinton alimuomba Biden mara hii asikubali kushindwa katika mazingira yoyote katika mbio za mwisho usiku wa uchaguzi.

Alielezea hali ambapo Warepublican wangelijaribu kuwatumia ujumbe wapigaji kura ambao hawajapiga kura na kutumia kundi la mawakili kupinga matokeo ya uchaguzi.

Senata Mitt Romney, alisema mapendekezo yoyote yanayoashiria rais huenda asiheshimu dhamana hii ya katiba hayaingii akilini na haiikubaliki.

Hofu juu ya uadilifu katika uchaguzi wa Novemba huenda ikawa ngome mpya ya makabiliano makali ya kisiasa sawia na suala la iwapo kuwa na jaji mpya wa mahakama ya juu zaidi kabla ama baada ya uchaguzi.

Mshindi wa uchaguzi wa November 3, ataapishwa rasmi Januari 20 mwakani.