NA KHAMISUU ABDALLAH

KATIBU Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Khamis Mussa, amesema lengo la serikali kuweka taa za kisasa za barabarani ni kuuweka mji katika haiba nzuri na kuimarisha usalama wa wananchi.

Kauli hiyo aliitoa wakati wa kusaini mkataba wa makabidhiano ya mradi wa uwekaji taa za kisasa wa awamu ya pili katika mkoa wa Mjini Magharibi hafla ambayo ilifanyika katika skuli ya sekondari Lumumba.

Alisema wapo baadhi ya madereva wamekuwa wakizifanyia hujuma taa hizo kwa kuzivunja kwa makusudi bila ya kujali serikali imetumia fedha nyingi katika uwekaji wa taa hizo.

Aidha alisema miundombinu hiyo iliyowekezwa kwa fedha nyingi kwa ajili ya usalama wa wananchi na wageni wanaoingia nchini, hivyo sio vyema kuihujumu kwa makusudi.

Akizitaja barabara zilizowekewa miundombinu hiyo, alisema ni barabara ya Mkapa kutoka Amani hadi Mtoni ambapo kilomita nne zimewekewa taa na barabara ya Malawi inayoanzia Malindi hadi Bububu kwa Nyanya kilomita 11.

Hivyo aliwaomba madereva na wananchi kuitunza miundombinu hiyo ili kutorejea kutumia fedha nyengine kuweka taa hizo ambazo zinawezekana kutunzwa kwa muda mrefu. 

Hata hivyo alibainisha kwamba serikali itaangalia uwezo wa kiuchumi ili kuweka taa hizo katika barabara za vijijini.  

Katibu huyo aliipongeza serikali ya Jamhuri ya watu wa China kwa kuendelea kuisaidia Zanzibar katika miradi mbalimbali ya maendeleo ukiwemo ujenzi wa hospitali ya Abdalla Mzee kisiwani Pemba.     

Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar, Xie Xiao Wu alisema serikali ya China itaendelea kuisaidia Zanzibar hasa katika shughuli za kijamii kutokana na uhusiano wa karibu uliopo kati ya Tanzania na nchi yake ulioasisiwa na viongozi wa nchi hizo.

Naibu Katibu Mkuu anaeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika wizara ya nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maluum za SMZ, Khalid Abdalla Omar akitoa maelezo mafupi ya kitaalamu alisema mfumo huo mpya wa taa za kisasa katika barabara ya Malawi na Mkapa zenye urefu wa kilomita 15.036 na kuweka jumla ya taa za kisasa 430.