“WAZEE ni hazina” Msemo huu ni maarufu kwa kuwa na maana kwamba kila jambo unalofanya ni lazima kumshirikisha mzee sio tu kupata baraka zake lakini uzoefu wake wa kujua mambo nao ni muihumu sana.
Tunaamini na ndivyo ilivyo hasa kuwa wazee ni rasilimali muhimu ya familia, jamii na taifa kwa ujumla ambayo inahitaji kutunzwa kwa nguvu zote kwani kuthaminiwa kwao kutawasaidia vijana kuchota busara, hekima, ujuzi na maarifa waliyonayo.
Kwa mantiki hiyo basi ndio maana Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikibeba dhima katika kuwaenzi na kuwathamini wazee jambo ambalo limewatengenezea ustawi mzuri.
Tangu uongozi wa marehemu Mzee Abeid Amani Karume, tumeshuhudia jinsi alivyowapa kipaumbele wazee kwa kuweza kuwatunza na kuwaenzi kwa kuwajengea nyumba maalum za kuishi na kuwapa huduma zote muhimu za kimaisha.
Fikra hizo za mzee Karume, zimekuwa zikitekelezwa kwa vitendo zaidi na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ya awamu ya saba ya Dk. Ali Mohamed Shein ambaye amewazidishi maradufu huduma stahiki wazee wa Zanzibar.
Katika kutekeleza hilo, ndipo tunapoiona hasa serikali ikiheshimu mchango wa wazee katika maendeleo yetu yaliyofikiwa kwa baada ya kukosa nguvu serikali inawatunza kwa kuwapa huduma za msingi.
Hatuna budi kuipongeza serikali kwa juhudi inazozichukua katika kuziimarisha huduma za kijamii na mahitaji muhimu wanayoyahitaji wazee wanaotunzwa katika nyumba za wazee za Unguja na Pemba.
Aidha tumeona kwa macho yetu jinsi serikali ya awamu ya saba, ilivyoanza kutekeleza mpango wa kuwapatia pencheni maalum wazee wote waliofikia umri wa miaka 70, mpango ambao ni nadra kutekelezwa na hata nchi tajiri duniani.
Uzuri wa pencheni hizo, hazina ubaguzi wa aina yoyote haziangalii jinsi, rangi, kabila na wala wapi mtu huyo anatokea ilimradi uwe umetimiza zaidi ya miaka 70, huu ndio msingi wa uendeshaji bora wa nchi ambapo Dk. Shein anatuonyesha.