“WAZEE ni hazina” Msemo huu ni maarufu kwa kuwa una maana kuwa kila jambo unalofanya ni lazima kumshirikisha mzee ili kupata Baraka zake.
Tunaamini na ndivyo ilivyo hasa kuwa wazee ni rasilimali muhimu ya familia, jamii na taifa kwa ujumla ambayo inahitaji kutunzwa kwa nguvu zote kwani kuthaminiwa kwao kutawasaidia vijana kuchota busara, hekima, ujuzi na maarifa waliyonayo.
Kwa mantiki hiyo basi ndio maana Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ikawa ina wathamini wazee kupita kiasi jambo ambalo hata limewatengenezea ustawi mzuri wazee.
Tokea uongozi wa Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, tumeshuhudia jinsi alivyowapa kipaumbele wazee kwa kuwatunza na kuwaenzi kwa kuwajengea nyumba maalum za kuishi pamoja na kuwapa huduma zote muhimu za kimaisha ili nao waweze kujisikia kuwa ni sehemu muhimu katika jamii.
Sote tunajua na kuona kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imewajengea nyumba za
makaazi wazee katika eneo la Sebleni mjini Unguja na Limbani Wete Pemba kwa
ajili ya kuwapatia huduma stahiki.
Tunaona kuwa Serikali inaheshimu mchango wa wazee katika maendeleo yetu pamoja na malezi na maadili mema wanayoyatoa kwenye jamii yetu.
Pamoja na mambo mengine, lakini hatuna budi kuipongeza serikali hasa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, ambapo serikali imeongeza juhudi katika kuziimarisha huduma za kijamii na mahitaji muhimu wanayoyahitaji wazee wanaotunzwa katika nyumba za wazee za Unguja na Pemba.
Aidha tumeona kwa macho yetu jinsi Serikali ilivyoanza kutekeleza Mpango wa kuwapatia pencheni ya shilingi 20,000 kwa wazee wote waliofikia umri wa miaka 70 bila ya kujali historia ya kazi walizokuwa wakizifanya, vyama wala maeneo wanayotoka.
Juhudi hizi za makusudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Dk. Shein ni muendelezo wa juhudi za viongozi wote walioiongoza Zanzibar tangu Mapinduzi ya mwaka 1964, katika kuimarisha ustawi wa wazee kwani tumeshuhudia kila awamu iliyopita jinsi ilivyolipa kipaumbele suala hili.
Zanzibar ni miongoni mwa nchi za kwanza Afrika kuwaenzi wazee kwa kuwajengea makaazi maalum lakini ni ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kuwapatia pensheni jamii, hivyo hatuna budi kuendeleza azma hiyo muhimu kwa ustawi wa wazee wetu.